Lissu Arusha Kombora Lingine kwa Mawaziri

Dodoma. Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Binilith Mahenge, jana walituhumiwa kutumia vibaya nafasi zao kwa kuweka fedha nyingi za miradi ya maji katika maeneo wanakotoka, huku sehemu zenye matatizo ya huduma hiyo zikitengewa fedha kiduchu.

Ilielezwa bungeni jana kuwa Profesa Maghembe ambaye ni Mbunge wa Mwanga, Kilimanjaro, wizara yake imetenga Sh1.4 bilioni kwa ajili ya miradi ya maji, ambazo ni zaidi ya mara saba ya Sh190 milioni zilizotengwa kwa ajili hiyo katika Wilaya ya Ikungi, Singida.

Akichangia Bajeti ya Wizara ya Maji jana, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alihoji kile alichokiita upendeleo wa wazi katika ugawaji wa fedha za maji, unaoipa kipaumbele baadhi ya mikoa wanakotoka mawaziri.

Pia aliitaja Wilaya ya Makete, Njombe anakotokea Dk Mahenge ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Maji kuwa imetengewa Sh1.9 bilioni na kusema: “Upendeleo wa aina hii haufai kwa sababu utaleta matatizo na siyo haki hata kidogo.”

“Profesa Maghembe atueleze sababu za kutenga bajeti hii kwa upendeleo, huku mikoa isiyokuwa na vyanzo vya maji, mito ya kudumu na mabwawa ya maana imepewa bajeti kidogo ikilinganishwa na ile yenye mifumo mizuri ya maji,” alisema Lissu.

Alisema licha ya Profesa Maghembe katika hotuba yake kutaja mikoa ya Dodoma, Singida, Simiyu na Shinyanga kuwa inakabiliwa na upungufu wa maji, imetengewa kiasi kidogo cha fedha, huku mikoa inayopata mvua za kutosha na vyanzo vya uhakika vya maji ikitengewa mabilioni ya fedha.

“Dodoma imetengewa Sh7.2 bilioni, Singida Sh3.2 bilioni, Shinyanga Sh3.2 bilioni na Simiyu Sh2.8 bilioni, wakati mikoa yenye vyanzo vya maji na mvua za kutosha imetengewa fedha nyingi; mfano ni Tanga Sh10.7 bilioni, Kilimanjaro Sh6.3 bilioni, Mbeya Sh9.2 bilioni na Mtwara Sh7.5 bilioni,” alisema.

Lissu alisema hali hiyo inaweza kutafsiriwa kuwa mawaziri hao wanatumia mamlaka yao kujipendelea na kuhoji kama huo ndiyo utaratibu wa Serikali ya CCM... “Kama utaratibu wa mgawanyo wa fedha ndiyo huu sisi tunaotoka mikoa yenye ukame tutapataje maji?”

Jana Profesa Maghembe aliendelea kuwa katika wakati mgumu, baada ya kuandamwa na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika ambaye alimwita kuwa ni mzigo kutokana na kutokutolewa kwa fedha za miradi ya maji.

Mnyika alionyesha kushangazwa na wabunge wenzake kuunga mkono bajeti ya wizara hiyo, licha ya kuwa ndogo na fedha za miradi zimekuwa hazitolewi kama inavyotakiwa.

“Kwa kufanya hivi sidhani kama tunamsaidia Profesa Maghembe ambaye ni CCM. Fedha zilizotengwa mwaka jana kuisaidia wizara hii hazijatoka na za bajeti hii hazitatoka kwa kiwango cha kuwezesha utekelezaji. Namna bora ya kumsaidia ili viongozi wa CCM wasiendelee kumwita mzigo ni kuikataa bajeti hii ili Serikali irudi mezani na kujiuliza.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad