Mawaziri Saba ‘Mahututi’

Msuguano mkali umekuwa wakati Bunge linapokaa kama kamati kupitia vifungu vya bajeti za wizara husika. Hata hivyo, bajeti hizo zimepitishwa baada ya maelezo marefu na wakati mwingine msaada wa kiti cha Spika au pale Waziri Mkuu au Kaimu wake ndani ya Bunge anaposimama ‘kuokoa jahazi’.

Mawaziri ambao hadi sasa wameingia katika orodha ya bajeti zao kupita kwa mbinde na wizara zao kwenye mabano ni Profesa Jumanne Maghembe (Maji), Profesa Anna Tibaijuka (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini), Dk John Magufuli (Ujenzi), Dk Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Sophia Simba (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto) na Dk Seif Rashid

(Afya na Ustawi wa Jamii).

Sababu za kasheshe

Kwa sehemu kubwa, bajeti nyingi zilipata upinzani kutokana na Hazina kutoa fedha kidogo za maendeleo kati ya asilimia 19 na 30 tu, wakati wizara nyingine zilitikiswa na tuhuma za ufisadi wa watendaji wake.

Sophia Simba

Miongoni mwa mivutano ni ule uliohusu taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama) ambayo Mwenyekiti wake ni mke wa Rais Jakaya Kikwete, Mama Salma, hoja iliyoibuka wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.

Mbunge wa Ole (CUF), Rajab Mbarouk Mohamed alitaka taasisi hiyo ifutwe, kwa maelezo kwamba inajihusisha na masuala ya kisiasa na kwamba mwaka 2010, Mama Salma aliitumia kumfanyia kampeni mumewe.

Katika hoja hiyo alisema mmoja wa wajumbe wa bodi ya taasisi hiyo ni Waziri wa wizara hiyo, Sophia Simba kinyume na sheria na taratibu.

Waziri Simba akajibu: “Nipo Wama lakini kazi ninayoifanya pale ni ya kujitolea na silipwi kitu. Kanuni na sheria zinakataza mtu kujihusisha na taasisi nyingine kama tu anakuwa analipwa mshahara”.

Profesa Maghembe

Juzi, Profesa Maghembe alipata wakati mgumu baada ya hoja iliyoshika mshahara wake iliyotolewa na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika kujadiliwa kwa dakika 31, hadi Kaimu Waziri Mkuu, Profesa Mark Mwandosya alipoingilia kati.

Wabunge bila kujali itikadi za vyama vyao, waliungana kutetea hoja ya kutaka suala la upatikanaji wa maji liwe ajenda ya kwanza ya Serikali. mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Pauline Gekul alitaka bajeti hiyo ifumuliwe ili kuondoa posho za vikao na safari.

Mbunge wa Lushoto (CCM), Henry Shekifu alisema tatizo la maji ni zito na akapendekeza kuanzishwa kwa mfuko wa maji.

Profesa Mwandosya alisimama na kutoa uthibitisho kwa niaba ya Serikali kwamba muswada huo wa fedha utapelekwa bungeni kabla ya kuvunjwa kwa Bunge 2015 na alikubaliana na wabunge kwamba suala la maji litakuwa ni nambari moja katika vipaumbele vya Serikali.

Dk Magufuli

Kauli ya Waziri wa Ujenzi, Dk Magufuli kwamba ujenzi wa barabara si sawa na chapati, ilisababisha baadhi ya wabunge kumjia juu wakati wa kupitisha vifungu vya bajeti ya wizara yake.

Baadhi ya wabunge wa mikoa ya kusini mwa nchi, walichachamaa kutokana kile walichodai kuwa ni kutotengwa kwa fedha za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.

Suala jingine lililotawala mjadala huo ni sakata la malori kuruhusiwa kuzidisha uzito barabarani, hoja ambayo iliibuliwa na Machali ambaye alimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwaomba radhi Watanzania kutokana na hatua yake ya kuyaruhusu kubeba mizigo mizito na kusababisha barabara zinazojengwa kwa mamilioni ya fedha za kodi za wananchi kuharibika. Pinda alitoa ufafanuzi mzuri.

Dk Mwakyembe

Wabunge walitaka maelezo ya kina juu ya uendeleshaji Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda), Shirika la Ndege (ATCL), ukarabati wa meli ya MV Victoria na upanuzi uwanja wa ndege Mwanza.

Wabunge waliokuwa vinara wa kupinga bajeti hiyo wakitaka mambo hayo manne kupatiwa ufumbuzi ni wabunge wa CCM, Dk Hamisi Kigwangalla (Nzega), Andrew Chenge (Bariadi Magharibi), Charles Mwijage (Muleba Kaskazini), Richard Ndassa(Sumve) na mbunge wa Ilemela (Chadema), Ezekiah Wenje.

Profesa Muhongo

Ni kati ya bajeti ambazo zilipita kwa mbinde huku wabunge wakiibua hoja na ufisadi mbalimbali uliofanywa ndani ya wizara hiyo.

Sakata la IPTL ni moja kati ya mambo yaliyotikisa mjadala wa bajeti hiyo huku Mnyika na mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka wakiwasilisha ushahidi kuhusu tuhuma kadhaa za wizara hiyo.

Mashambulizi hayo yaliibua tuhuma mpya dhidi ya wabunge, Profesa Muhongo alipodai kwamba baadhi ya wabunge wakiwamo wa upinzani wamehongwa na IPTL.

Katika maelezo yake, Profesa Muhongo alisema ana ushahidi wa kamera za CCTV zinazowaonyesha vigogo hao wa upinzani wakisaini nyaraka na kuchukua fedha hizo.

Sakata jingine lililoibuka ni kukosekana kwa umeme katika maeneo ya vijijini na kulazimika Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutoa ufafanuzi akisema kuwa fedha zitakazotengwa kwa ajili ya Mfuko wa Nishati Vijijini (Rea) hazitaguswa.

Profesa Tibaijuka

Waziri Tibaijuka alijikuta katika wakati mgumu baada ya wabunge, wengi wa Dar es Salaam kumbana kuhusu ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni.

Suala hilo lililohusishwa na ufisadi lilionekana kumchanganya waziri huyo na wakati mwingine alishindwa kujibu maswali na badala yake kuwashambulia wabunge wa upinzani hasa Halima Mdee wa Chadema.

Alisema wapo wabunge ambao walikuwa na hoja na wengine walikuwa wakipiga kelele, akitoa mfano tuhuma dhidi yake kuwa anamiliki kiwanja katika Mji wa Kigamboni kwamba hazina ukweli wowote.

Dk Seif Rashid

Nayo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilikumbwa na dhoruba jana kabla ya kuokolewa na Profesa Mwandosya baada ya wabunge wengi hususan wanawake, kutaka kuikwamisha.

Imeandikwa na Daniel Mjema, Fidelis Butahe na Habel Chidawali
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. nilitaka list ya hao mawaziri 7 ambao wako hoi, ww admin mbona uelewek kichwa cha habari ni tofauti na maelezo yako? Mamamaaaaeeeeeee

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad