Nape Amfyatua Mwigulu kuhusu Bunge la Katiba

SIKU moja baada ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Mwigulu Nchemba kunukuliwa na gazeti la serikali la Habari Leo akitamba kupinga nyongeza ya siku 60 za Bunge la Katiba, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, amempinga akisema hawezi.

Mwigulu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, alitoa tambo hizo juzi mjini Iringa wakati akihutubia mkutano wa hadhara, akisema kuwa atapinga kwa nguvu zake zote Bunge hilo kukutana kwa siku nyingine 60.

Hata hivyo, msimamo wake unakinzana na chama chake ambacho kimeapa kwamba hata kama wajumbe wenzao wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wasiporudi bungeni, wao wataendelea na Bunge hadi katiba mpya ipatikane.

Katika kikao chake cha Kamati Kuu cha hivi karibuni, CCM iliazimia kupambana na UKAWA popote, nje na ndani ya Bunge Maalumu la Katiba, huku ikisisitiza kwamba haiwezi kuwabembeleza warudi bungeni kwa sababu chama hicho kinao wajumbe wa kutosha kutimiza theluthi mbili ya kura zinazotakiwa kikanuni.

Kufuatia mkorogano huo, Tanzania Daima Jumatano lilimtafuta Nape jana kwa simu akiwa ziarani mkoani Manyara ili kupata msimamo wa chama kuhusu katiba mpya.

Katika majibu yake kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu, Nape alisema: “Gazeti la Habari Leo limemnukuu vibaya Mwigulu. Hawezi kupinga jambo ambalo rais amelipitisha.

“Chama kupitia vikao halali kimeishatoa tamko na msimamo unajulikana. Vinginevyo ili ampinge rais, yeye kama naibu waziri alipaswa ajiuzulu kwanza. Hata hivyo, naibu waziri haruhusiwi kuwasilisha hoja binafsi.”

Kwa mkanganyiko huo, ni dhahiri CCM wanakinzana katika suala zima la upatikanaji wa katiba mpya inayotokana na matakwa ya wananchi.

Itakumbukwa kuwa katika siku za hivi karibuni kwenye mikutano yao ya hadhara iliyofanyika visiwani Zanzibar na mkoani Tabora, CCM kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana na Nape walisema kuwa hawahitaji katiba mpya kwa sababu sio muarobaini wa matatizo waliyonayo wananchi.

Viongozi hao walisisitiza kuwa hata katiba mpya ikipatikana itawekwa kabatini, huku Nape akizidi kuwashambulia wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, akisema wamekengeuka kwa mapendekezo yao ya muundo wa serikali tatu.

Licha ya rasimu ya katiba kupendekeza muundo wa serikali tatu, CCM imekuwa ikiendesha harakati za kuipindua, ikitetea muundo wa sasa wa serikali mbili uendelee, jambo linalopingwa na UKAWA hadi kufikia hatua ya kutoka nje ya Bunge hilo.

Katika mkutano wake wa mjini Iringa, Mwigulu alipinga Bunge hilo lisiongezewe muda kwa madai kwamba likiendelea kwa mtindo kama wa awamu ya kwanza, itakuwa sawa na kutumia vibaya fedha ya walipa kodi.

Aliahidi kumshauri Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, amuandikie barua Rais Jakaya Kikwete, ili avunje Bunge hilo endapo wajumbe wake watashindwa kutumia wiki mbili za mwanzo kujadili mambo ya msingi katika rasimu hiyo.

Source: Tanzania Daima
Tags

Post a Comment

7 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. ktk baraza la mawaziri mwigulu asingestahili kuwepo.mara nyingi anakurupuka.anaongeaga pasipo kufikiri..nadhani hata baadhi ya wabunge wenzake wanamshangaa..ABADILIKE NA AJITAMBUE

    ReplyDelete
  2. mwigulu ndo bogus kabisaaa jakaya kambeba tu

    ReplyDelete
  3. Mwigulu alizaliwa kabla ya wakati( mtoto njiti) kuna vitu havimtimia.

    ReplyDelete
  4. Lkn sifa za kuongoza anazo jaman

    ReplyDelete
    Replies
    1. Kama zipi wewe tango pori?

      Delete
  5. Hana ndio maana umeambiwa rais amembeba tu. Anachoweza ni kuwapiga vijembe upinzani na sio kutengeneza hoja

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad