Kilichotokea mnadani
Katika eneo la mnada wa kuuza vitu vya machinga vilivyokamatwa lililopo katika Soko la Kibasila Gerezani, kulikuwa na makundi ya watu wa aina mbili; waliokwenda kununua vitu vingi kwa bei ndogo na wengine ni wale ambao bidhaa zao ndizo zilikuwa zinapigwa mnada na hawakuwa na uwezo wa kushinikiza wauziwe wao.
Wafanyabiashara waliokuwapo katika eneo hilo jana, walisikika wakisema wamekwenda kununua vitu vya dhuluma na kwamba walilazimika kununua kwa kuwa hakukuwa na njia nyingine ya kufanya.
Leonard Mwagike alisema baada ya bidhaa zake kukamatwa alijaribu kwenda kuzikomboa lakini alishindwa baada ya Mahakama ya Jiji kumwamuru alipe faini ya Sh400,000.
“Kinachoendelea hapa ni dhuluma tu, haiwezekani mzigo wangu wa Sh50,000 uniambie nilipe faini ya Sh400, 000, bora kuja hapa kuununua tena kama nitaweza,” alisema kwa huzuni.
Mfanyakazi wa kampuni moja ya udalali jijini, iliyopewa mamlaka ya kuuza bidhaa hizo, alikuwa akifungua mzigo mmoja baada ya mwingine na kuwataka wafanyabiashara hao wapange bei.
Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida, alionekana kutaka kuchukua kila bidhaa aliyoiona ni nzuri, huku akiwaambia wanunuzi kuwa alikwishaichunguza mizigo hiyo kwa hiyo anajua upi ni mzuri.
Mzigo wa kwanza kufunguliwa ulikuwa una vyombo vya plastiki vya kuwekea chakula, ambavyo vyote viliuzwa kwa Sh10, 000. Zilifuata nguo za watoto na chupa za chai, kisha ukafika wakati ulioleta msuguano kiasi cha kutishia mnada kuvunjika.
“Sasa kwenye mzigo huu kuna mali nzuri wengine wameshaiona si ndiyo? Eeh! Ni madera (magauni), mfuko mzima shilingi ngapi?” Anauliza dalali, lakini kabla hajapata jibu anasema:
“Jamani yupo shemeji yenu (mke wake) lazima naye apate hizi nguo (huku minong’ono ikianza kusikika anachukua magauni matatu na kuyaweka pembeni).”
Kitendo hicho kiliwakasirisha baadhi ya machinga waliokuwapo katika eneo hilo, huku wakisema iwapo angeuona mapema mzigo huo angeuchukua wote.
“Mali mmetunyanganya sisi na hata tunazonunua hapa mtazichukua tena, halafu bado mnachukua hata mnazouza, hili halikubaliki,” alisema mfanyabiashara mmoja.
Baada ya kuuzwa kwa bidhaa mbalimbali zikiwamo feni, viatu na suruali, linapatikana tena furushi lenye madera na hali ikawa kama ilivyokuwa awali.
Dalali: “Ule mzigo huu hapa tena, lakini saa hizi tuuweke pembeni kwanza, mimi ninaweza kuuchukua wote.” Kauli hiyo inapingwa huku kila mtu akitaka magauni yote yahesabiwe.
Wakati uuzaji ukiendelea, Mmachinga mmojawapo anabaini kuwa mzigo wake uliokuwa umekamatwa umeuzwa kwa mtu mwingine hivyo anaamua kumfuata na kuongea naye.
“Haiwezekani mzigo wangu mkubwa vile wa mikoba anunue mtu kwa Sh8,000 tu,” anasema huku akiondoka.
Hamisi Kiwanuka anasema alikamatwa kwa kosa la kupanga na kuuza feni barabarani, lakini alipojaribu kuzitafuta baadaye hakuzipata, badala yake aliziona nyingine zimevunjika, ambazo hazikuwa zake.
“Hawa jamaa wanauza hapa vitu vilivyobaki baada ya kuchambuliwa sana, vizuri vyote wamechukua,” alisema.
Pia, mama mmoja aliyetambuliwa kwa jina moja la Mama Kuluthumu, ambaye alifanikiwa kununua sufuria 17 kwa sh10, 000, alisema:
“Baadhi ya sufuria ziliondoka na wali na nyama sijui ziko wapi?”
Viongozi wanena
Mwenyekiti wa Operesheni ya kuwaondoa Wamachinga barabarani jijini hapa, Msongoro Songoro, alisema wapo wafanyabiashara wa aina mbili ambao wanalengwa katika zoezi hilo la safisha jiji; wanaotoa bidhaa ndani ya maduka na kuzipanga nje na wale wanaoweka barabarani.
Wafanyabiashara wanaopatikana na kosa la kupanga bidhaa nje hutozwa faini ya papo kwa papo ya Sh50, 000 na kupewa onyo, ambapo fedha inayopatikana hupelekwa katika halmashauri husika na zile zinazopatikana kwenye mnada hupelekwa ofisi ya jiji.
“Lakini anayepanga bidhaa barabarani, akikamatwa anafikishwa mahakamani na mali yake inataifishwa kwa sababu hana leseni ya kufanya biashara hiyo,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema hadi kufikia Juni 12 mwaka huu jumla ya wafanyabiashara 711 walifikishwa mahakamani, huku baadhi yao wakihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja au faini kati ya Sh100,000 na Sh400, 000.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma za askari wa Jiji kula chakula cha wafanyabiashara, Songoro alisema kuwa taarifa hizo siyo za kweli kwa sababu kutokana na vurugu zinazokuwapo wakati wa ukamataji siyo rahisi chakula hicho kufaa kuliwa tena.