Sakata la nani mmiliki halali wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda), limeendelea kuchukua sura mpya. Wakati Mbunge wa Temeke (CCM), Abbas Mtemvu akitoa tuhuma kwamba limeuzwa kinyemela, Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Simon Group, Robert Kisena ameibuka na kudai kuwa halikuwahi kuuzwa.
Juzi, akichangia mjadala wa Bajeti wa Wizara ya Fedha, Mtemvu alisema kulifanyika ujanjaujanja kati ya Simon Group na Meya wa Jiji, Didas Masaburi kukopa benki na taasisi nyingine kwa ajili ya kununua kampuni hiyo.
Mtemvu alisema baada ya Simon Group kuuziwa Uda kwa bei poa, wahusika walishindwa kulipa fedha hizo ndipo (wadai) walipokwenda mahakamani na kutaka walipwe chao.
Alisema baada ya kampuni na benki walizokopa kushinda kesi mahakamani, kampuni moja ya udalali ilipewa kazi ya kuipiga mnada depo ya Uda na Februari 23, ilinunuliwa na Jazeera kwa Sh12bilioni.
Jana, Mtemvu alisema: “Tunaambiwa kulikuwa na zuio, hapa tunataka kujua, kwanza huyu aliyeweka hati za Uda kwa zuio isipigwe mnada... utaratibu uliotumika kuiuza Uda, hapa kuna mchezo mchafu umefanyika, iweje mambo yafanyike bila wadau, wahusika wa mkoa kushirikishwa?”
Alisema Uda haiwezi kuuzwa kwa bei chee ya Sh280 milioni... “Ina viwanja Stesheni, ina nyumba Msasani, Chang’ombe, Ilala Sharif Shamba, Kijitonyama, Upanga hivi vyote ni zaidi ya Sh280 milioni.”
Katika maelezo yake bungeni juzi, Mtemvu alisema wabunge wa Dar es Salaam hawakatai kubinafsishwa kwa Uda ila wanataka uhalali na haki katika ubinafsishaji huo.
Kisena
Akizungumza jana, Kisena alisema Uda haijauzwa na hawana mpango wa kuiuza na akahusisha tuhuma hizo na mkakati mbaya unaofanywa na baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya shirika hilo.
“Mimi ndiyo kwanza nasikia habari hizo eti Uda imeuzwa kwa Kampuni ya Jazeera… sijui kwa nani… huo ni uzushi.
Nenda kwa Mtemvu akupe document (nyaraka) za uuzwaji wa Uda… akwambie iliuzwa lini na kwa sababu zipi na kama iliuzwa kwa madeni ni benki gani inadai ili uweze kufuatilia na kuuambia umma ukweli.”
“Watu wote watambue kuwa Uda inamilikiwa na watu wawili: Simon Group na Serikali kupitia Msajili wa Hazina na hakuna mmiliki mwingine na halijauzwa. Hii kampuni ni kubwa sana hivi iuzwe bila waandishi wa habari na umma kujua na mnada hutangazwa siku 14 kabla… yaani siku zote zipite watu wasijue?” alihoji Kisena.
Brela
wakati mvutano huo ukiendelea, Wakala wa Usajili na Utoaji wa Leseni za Biashara (Brela), umesema hauna taarifa zozote za kampuni hiyo kuuzwa.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Frank Kanyus alisema jana kuwa ofisi yake haina nyaraka zozote zilikuwa zikionyesha Uda kuwa iliuzwa kwa Kampuni ya Jazeera.
“Tulisikia taarifa hizo lakini hatukupata document (nyaraka) zozote zinazothibitisha jambo hilo. Nimewaomba maofisa wangu waendelee kufutilia suala hilo na kama kuna chochote tutawajulisha,” alisema Kanyus.
Sakata la Uda liliibuka tena juzi kwa Mtemvu na Mbunge wa Urambo Magharibi (CCM), Profesa Juma Kapuya kuchafua hali ya hewa bungeni kila mmoja akimtuhumu mwenzake kuwa anahongwa kutetea ufisadi katika shirika hilo.
Mvutano huo umeibuka wakati Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge ikiwa tayari imemhoji, Kisena baada ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika kusema aliingilia uhuru wa Bunge kuhusu mgogoro wa uwekezaji katika shirika hilo.
Juzi bungeni
Juzi bungeni, Mtemvu alisema: “Kwanza niseme kitu kimoja kibaya sana, humu ndani kuna mjumbe wa Bodi ya Uda (Profesa Kapuya), alikuwa akizunguka sana humu ndani (ndani ya Bunge) huku akiwaona wa wabunge kitendo hicho si kizuri.”
Alisema kuwa mwekezaji huyo wa Uda ameliuza shirika hilo kwa Sh280 milioni na kuhoji kama kiasi hicho cha fedha ni hadhi ya Uda na kuwa mwekezaji huyo hakukabidhiwa shirika hilo na vikao halali vya jiji la Dar es Salaam, bali na Meya wa Jiji.
“Tunapoongea tusiangalie sambusa za Dodoma Hotel, tuangalie uasilia wa jambo, hivi tunauza mali ya Serikali bila Baraza la Mawaziri kujua?” alihoji.
Mtemvu alikatishwa na taarifa kutoka kwa Profesa Kapuya ambaye alisema si haramu kwa mbunge kuwa mwekezaji.
“Sera inaruhusu kwa mbunge kuwa mfanyabiashara. Afadhali mimi nimezunguka kuona watu kuliko anayezunguka kwa madhumuni ya kurudisha imprest (masurufu),” alisema Profesa Kapuya.
“Na aliyezungumza ni mmojawapo (Mtemvu)… hakuna mali ya Serikali iliyouzwa bila idhini ya Baraza la Mawaziri, zilizouzwa ni hisa za jiji ambazo yeye alikuwemo katika kikao (Mtemvu)”alisema.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Sharon Sauwa, Habel Chidawali (Dodoma) na Nuzulack
jilieni tu kwani mnashida gani lkn kwa mungu mtakoma
ReplyDeletenchi hii wanafaidika wachache wenye kujua kutafuna, ila majib kwa allah mtayajib cku ya mwisho
ReplyDeleteNashangaa sna....hayo mahela kula wale wao alafu kubishana wabishane wao.....kweli wanatufanya....wajinga
ReplyDeleteSiku za mwisho watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe kuliko kumpenda mungu
ReplyDelete