Ukamataji Wanaodai Kutibu Ukimwi Ufanywe kwa Vitendo

MATANGAZO ya watu mbalimbali kuibuka na kudai kutibu magonjwa mbalimbali yamekuwa yakiongezeka kadri siku zinavyosonga mbele kwa kubandikwa mitaani pamoja na kutangazwa sehemu mbalimbali.

Suala hili, limezidi kushika kasi kutokana na ukweli kuwa kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza kama kisukari, presha, magonjwa ya figo pamoja na mengineyo.

Vyombo vya habari vimekuwa na mchango mkubwa katika kuwatangaza watu hawa bila kutambua iwapo dawa hizo zimethibitishwa au hapana jambo ambalo ni hatari kwa afya za wananchi.

Watu hawa wamekuwa wakitumia mianya ya magonjwa hayo ukiwemo Ukimwi kwa kujipatia fedha mbalimbali kwa kulipia matangazo hayo katika vyombo vya habari na kutangazwa jambo linalofanya watu kuamini kuwa iwapo limetangazwa ni wazi limepitishwa kutibu magonjwa mbalimbali.

Hivyo, ni vema Wizara ya Afya ambayo imetangaza bungeni kuviagiza vyombo vya dola, kukamata waganga wa jadi, wanaojitangaza kutibu magonjwa ya Ukimwi, kisukari na shinikizo la damu.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid aliwasihi wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala, kuacha mara moja, kujitangaza kuwa na uwezo wa kutoa tiba dhidi ya ugonjwa wowote ule ambao uwezo huo haujathibitishwa kitaalamu.

Alisema hilo ni kosa kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha tiba asili na tiba mbadala, na kutaka matangazo hayo yaondolewe mara moja.

Utata wa suala hili, linakuja ni jinsi gani wananchi wanaweza kutambua tiba iliyoidhinishwa kitaalamu na ambayo haijaidhinishwa ili vituo vya redio viweze kutangaza ambazo zimeidhinishwa.

Kutokana na changamoto hiyo, bado wizara husika ina kazi katika kusaidia kutoa elimu stahili kwa wananchi juu ya dawa hizo kwani wote tunaamini mtu anapokuwa akisumbuliwa na magonjwa anahangaika kupata tiba.

Ni vema wizara kwa kutumia wataalamu wake kuwa na kitambulisho maalumu kwa vyombo vya habari kutangaza matangazo ya dawa husika ili wanapotaka kutangaza kuhakikisha yameidhinishwa na Serikali.

Pia ni vema, suala hilo la kuwakamata waganga hawa wanaojitangaza kufanyika kwa vitendo kwani kwa muda mrefu tumekuwa tukisikia kauli hizo lakini bado matangazo mitaani ya kwenye vyombo vya habari yakiendelea.

Kuendelea kwa wizara kutoa matamko bila kutumia vitendo ni sawa na kazi bure kwani watu hao wamekuwa wakiongezeka kwa muda kadhaa na kuwachanganya wananchi jambo ambalo wanafanya kwa uwazi hivyo ni rahisi kuwachukulia hatua.

Kwani ikiwa wanatumia vyombo vya habari wanaelekeza mpaka mahali wanapotolea huduma hizo na hata katika matangazo wanayobandika barabarani pia wanajielekeza walipo sasa jambo la kushangaza ni nini kinachokwamisha katika kuwakamata?

Pia, ninashauri kuwa katika kukabiliana na watu hawa hatari kwa afya za Watanzania kwani kwa kuwadanganya kutibu magonjwa mbalimbali hufanya wagonjwa kuacha kutumia dawa stahili ni vema elimu ikatolewa kwa nguvu zote.

Pia Wizara ingeshirikiana na manispaa zote za miji kuhakikisha wanaondoa matangazo yote yaliyobandikwa mitaani na kisha kuwachukulia hatua watu hao kwa kuwalipa vijana watakaowekwa kuangalia mabango hayo na kuyaondoa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad