Wizi NMB Mwanga: Wakenya Wawili Wahukumiwa Kifo

Raia wawili wa Kenya, Samweli Saitoti (Saimoo) na Michael Kimani (Mike), wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), PC Michael Milanzi mwaka 2007.

Raia hao ambao walipambana na polisi jijini Arusha kwa saa sita wakijihami kwa silaha za kivita yakiwamo mabomu ya kurusha kwa mkono na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG), walifanya mauaji hayo yaliyoambatana na uporaji wa Sh239 milioni mali ya Benki ya NMB, Julai 11, 2007.

Pia, Jaji Kakusulo Sambo wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, amemhukumu Mtanzania, Calist Kanje kwenda jela miaka mitano kwa kuwasaidia wauaji hao wasikamatwe na polisi baada ya kufanya mauaji.

Akitoa hukumu hiyo jana, Jaji Sambo alisema upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya, Stella Majaliwa na Ignas Mwinuka, umethibitisha mashtaka hayo pasipo shaka.

Jaji Sambo alisema ushahidi wa mashahidi 18, umethibitisha kuwa raia hao wa Kenya ndiyo walioshirikiana kwa pamoja, kumuua polisi huyo ambaye taifa bado lilikuwa likihitaji utumishi wake.

“Kulikuwa na hoja ya utetezi kuwa hawakutambuliwa kikamilifu lakini PC Naftali Ashery aliyekuwa lindo na marehemu aliwatambua vilivyo wauaji hao tena kwa ukaribu,” alisema. Alisema Mahakama imeridhika kuwa maungamo waliyoyatoa mbele ya walinzi wa amani ambao ni mahakimu waliyatoa kwa hiari bila kushurutishwa.

Mahakama imeukataa utetezi wa washtakiwa hao kuwa wakati wa mauaji hawakuwa nchini, akisema ushahidi wa vinasaba (DNA), umethibitisha walikuwapo nyumbani kwa mshtakiwa Kanje.

Jaji alisema kwa kuwa washtakiwa hao walikwenda kwa Kanje na yeye akawasaidia wasikamatwe na kuwatorosha, hilo ni kosa la kusaidia wahalifu baada ya kufanya mauaji.

Jaji Sambo alisema Kanje ndiye aliyeficha gari aina ya Toyota Land Cruiser mali ya Mahakama ya Kimataifa ya Rwanda (ICTR), lililotumika katika ujambazi huo na kwamba ushahidi wa wafanyakazi wawili wa mshtakiwa huyo, unathibitisha kuwa ndiye aliyetoa maelekezo kwa dereva wake ili akalitelekeze gari hilo eneo la Uwanja wa Ndege wa KIA.

Mahakama hiyo imeamuru kiasi cha fedha, Dola 8,145 za Marekani na Sh1,769,000 walizokutwa nazo raia hao wa Kenya, zikabidhiwe Benki ya NMB, Mwanga zilikoibwa.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. 2007 na saba mpaka leo miaka 7 imepita kesi ndo inahukumiwa, jamani hii nchi maana hapo kama mashaihidi washakufa, ni shida

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad