Brazil Wamtupia Virago Kocha Scolari Baada ya Kichapo cha Saba Moja

Hatimae shirikisho la soka nchini Brazil CBF, limemjibu kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo Luiz Felipe Scolari, kwa kumuarifu halitomsainisha mkataba mpya.

CBF wametoa tamko hilo, baada ya Scolari kutamka hatojiuzulu kufuatia matokeo mabovu aliyoyapata wakati wa fainali za kombe la dunia, na badala yake anauachia uongozi wa shirikisho la soka nchini Brazil kufanya maamuzi.

Mapema hii leo kituo cha Televisheni cha Globo TV, kimeripoti kwamba uongozi wa CBF hautokuwa tayari kumpa mkataba mpya Scolari na badala yake wamemuamuru kuondoka kwenye kiti cha ukocha wa timu ya taifa ya Brazil.

Maamuzi hayo yamekuja kufuatia aibu kubwa iliyoikuta timu ya taifa ya Brazil mwanzoni mwa juma lililopita, ambapo ilikubali kufungwa mabao saba kwa moja na timu ya taifa ya Ujerumani, na kutolewa kwenye michuano ya kombe la dunia katika hatua ya nusu fainali.

Mchezo wa kumsaka mshindi wa tatu, pia ulishuhudia mabingwa hao mara tano wa dunia, wakipoteza mbele ya Uholanzi kwa kukubali kichapo cha mabao matatu kwa sifuri hali ambayo iliwazidishia hasira mashabiki wa soka nchini Brazil.

Kufungwa kwa Brazil katika michuano ya kombe la dunia ambayo ilifanyika nchini kwao, kunaifanya nchi hiyo kupoteza mchezo katika ardhi ya nyumbani kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1975.

Scolari aliwahi kuiongoza timu ya taifa ya Brazil na kutwaa ubingwa wa kombe la dunia mwaka 2002, baada ya kuifunga timu ya taifa ya Ujerumani mabao mawili kwa sifuri katika mchezo wa hatua ya fainali.

Tangu aliporejea kuwa kocha wa Brazil mwaka 2013, The Canarinho wamefanikiwa kushinda michezo 19, wamepata matokeo ya sare mara sita na kupoteza michezo minne.

Hata hivyo Scolari, aliiongoza vyema timu ya taifa ya Brazil katika michuano ya kombe la mabara ya mwaka 2013, iliyofanyika nchini Brazil na kufanikiwa kutwaa ubingwa.

Tayari aliyekua kocha wa klabu ya Corinthians, Tite, meneja wa klabu ya Sao Paulo Muricy Ramalho pamoja na kocha wa timu ya taifa ya Brazil chini ya umri wa miaka 20 Gallo wameanza kutajwa katika kuwania nafasi iliyoachwa wazi na Scolari

Quote of The Day:
“You can't depend on your eyes when your imagination is out of focus.” 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad