Jua Kuhusu Viungo vya Binadamu Ambayo Hutumika Kufundishia Madaktari.

Wakati sakata la kuokotwa kwa viungo vya binadamu likiendelea kutikisa nchi, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kimesema kuwa hutumia maiti 25 kwa kuwafundishia wanafunzi kila mwaka.

Pia chuo hicho hakijawahi kuagiza maiti kutoka nje ya nchi na kwamba ni mtu mmoja tu aliyewahi kutaka maiti ya mtoto wake itumike kufundishia.

Kauli hiyo ya MUHAS imekuja siku chache baada ya Serikali kuamua kuifungia Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), baada ya kubaini kasoro kadhaa katika utendaji wake.

Juzi, Serikali ilifanya ukaguzi wa kushtukiza IMTU, baada ya hospitali hiyo kukumbwa na kashfa ya utupaji wa mabaki ya viungo vya binadamu katika Bonde la Mto Mpiji, jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki iliyopita.

Hata hivyo, wakati Tume ya Watu 15 iliyoundwa na Serikali kuchunguza suala hilo ikiendelea na kazi, Mkuu wa Kitengo cha Anatomy MUHAS, Profesa David Ngassapa amebainisha kuwa chuo hicho hutumia maiti 25 kwa mwaka.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Ngassapa alisema kuwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza hutumia maiti 20, huku madaktari wanaorudi chuoni hapo kwa ajili ya mazoezi wakitumia maiti tano.

“Sheria ya mwaka 1963 inatutaka baada ya matumizi tuondoe mwili kwa heshima zote na miongoni mwa vitu ambavyo wanafunzi wanasisitizwa ni kuhakikisha wanaiheshimu miili hadi hatua za mwisho,” alisema Ngassapa.

Alieleza kuwa pamoja na sheria kutoa ruhusa ya kutumia maiti katika mafunzo, bado imeweka vipengele vinavyowataka madaktari kuiheshimu miili ya watu, hadi hatua ya mwisho.

Ngassapa aliongeza: “Sheria inaruhusu kuhifadhi mabaki ya miili kwa njia mbili; kuizika na kuichoma moto, pia hospitali inaweza kuhifadhi mabaki hayo hata kwa miaka mitano.”

Hajawahi kuagiza miili kutoka nje. 
Akizungumzia utaratibu wa nchi kubadilishana maiti kwa ajili ya mafunzo, Profesa huyo alisema kuwa kwa zaidi ya miaka 30 aliyokuwa katika kitengo hicho, hawajawahi kuagiza maiti kutoka nje ya nchi.

Alisema maiti zilizopo nchini zinatosha kufundishia wanafunzi wote wa udaktari kwa kuwa siyo Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH), pekee inayotegemewa kutoa miili hiyo.

Alisema kuwa siku za nyuma, Serikali ilikuwa ikiagiza mifupa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya mafunzo, lakini sasa kila kitu kinafanyika hapa nchini.

Ngassapa alisema kuwa miili iliyoharibika kwa ajali au magonjwa haifai kutumiwa kwa kuwa mwanafunzi anatakiwa kujifunza kwenye mwili uliokamilika.

Amkumbuka mtu aliyetoa maiti ya binti yake. 
Alisema kuwa historia ya Tanzania inaonyesha kuwa ni mtu mmoja pekee ndiye aliwahi kujitolea maiti ya binti yake ili itumike kufundishia.

“Alijitolea kwa kuwa binti yake huyo alianza kuugua akiwa na umri wa miaka miwili hadi alipofikisha miaka 12, muda mwingi akiwa amelazwa hospitalini hapa,” alisema.

“Alipofariki dunia mzazi alisema mtoto huyo ni wa hospitali na anamtoa kwa ajili ya matumizi ya hapa. Ibada ya mazishi ilifanyika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti,” alisema Ngassapa.

Alifafanua kuwa hata baada ya kukabidhiwa maiti hiyo, waliendelea kumhifadhi kwa miaka minne, hadi walipojiridhisha kuwa wazazi hawatabadilisha mawazo.

Sheria inayotumika 
Mkuu huyo wa kitengo kinachoshughulikia mwili na viungo vyake, alisema kuwa sheria ya Serikali ya mwaka 1963, ndiyo inayoruhusu chuo chochote cha afya kuchukua mwili kama umekaa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa siku 14 bila ndugu kujitokeza.

Ngassapa alifafanua kuwa licha ya sheria kuwataka kuchukua mwili uliokaa katika kipindi hicho, chuo huuhifadhi mwili huo kwa siku 30, ili kujiridhisha pasipo shaka kwamba hakuna ndugu anayejitokeza kuuchukua.

Alibainisha kuwa baada ya hapo, huuweka dawa ili usiharibike, kisha huuacha kwa wiki mbili au tatu zaidi wakisubiri kama ndugu wanaweza kujitokeza.

“Inapothibitika kuwa hakuna anayejitokeza, chuo huuchukua na kuutumia kwenye mafunzo,” alisema.

Alifafanua kuwa sheria pia inakitaka Kitengo cha Anatomy kuandika barua kwa mkuu wa chuo na Mahakama Kuu, kutaarifu kuwa wamechukua mwili kutoka katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Primus Saidia juzi aliliambia gazeti hili kuwa miili ni mali ya Serikali na kwamba chochote kinachofanyika kwa binadamu lazima kifuate sheria zilizowekwa na Serikali.

Pia alisema kwamba sheria inaruhusu nchi kubadilishana maiti, lakini hana uhakika kama jambo hilo limewahi kufanyika nchini, ingawa ana uhakika kuwa haiwezekani hospitali zikakosa maiti za kufundishia.MWANANCHI

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad