SIKU chache baada ya kukutwa mauzauza katika kaburi la mwigizaji Rachel Haule ‘Recho’, kaburi la mwigizaji Adam Kuambiana (pichani)limekutwa limetoboka kimaajabu.
Gazeti la Risasi Jumamosi toleo la Julai 19, mwaka huu lilikuwa na babari yenye kichwa cha habari kisemacho: ‘Uchawi kaburini kwa Recho.’ Kwenye habari hiyo, ilielezwa kuwa katika kaburi la Recho kulikutwa tunguri iliyoviringishwa shanga, kitambaa cha kanga chakavu, manyoya ya kuku, yai moja na vitu vingine ambavyo havikujulikana ni nini.
Baada ya habari hiyo, siku mbili baadaye, chanzo kingine kiliwapigia simu waandishi wetu na kuwaeleza kuwa mbali na tukio la Recho, kaburi la Kuambiana limetoboka kimaajabu na kuzua mtafaruku miongoni mwa watu walioshuhudia kwa mara ya kwanza tukio hilo.
“Jamani haya ni mambo ya kishirikina, huwezi amini kaburi hili limetoboka ghafla kimaajabu maana juzi tu nilikuja kutembelea makaburi haya, lilikuwa halijatoboka,” kilisema chanzo hicho.
Mapaparazi wetu walifika katika makaburi hayo na kujionea kaburi hilo likiwa limetoboka huku watu wengi waliokuwepo eneo hilo walidai kuwa tukio hilo si la kawaida kwani limetokea wakati ambao mvua hazijanyesha.
Walisema kama tukio hilo lingetokea wakati ambao mvua zinanyesha basi wasingekuwa na mashaka lakini kwa jinsi ambavyo limetoboka wakati wa jua kali ni dhahiri kutakuwa na ‘mkono wa mtu’.
“Hapa bwana tusidanganyane kuna mkono wa mtu, haiwezekani kaburi lisitoboke kipindi kile cha mwanzomwanzo lije kutoboka sasa wakati kuna jua kali namna hii, lazima kuna mkono wa mtu tu,” alisema shuhuda mmoja.
Wengine walikwenda mbali zaidi kwa kuhoji kulikoni matukio hayo yawe kwa mastaa pekee na si kwa watu wengine?“Hii si bure hapa wachawi watakuwa na shida yao binafsi, haiwezekani iwe kwa mastaa tu ndiyo kunakuwa na mauzauza,” alisikika shuhuda mwingine.
Alipoulizwa mmoja wa walinzi wa eneo hilo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema hata yeye hajui kwa nini inatokea katika makaburi ya mastaa.“Mimi hata sijui kwa nini lakini yamefululiza, juzi tumeona kwa Recho na leo kwa Kuambiana, tumuombe sana Mungu atuepushe na mabaya,” alisema mlinzi huyo.
Hata hivyo, licha ya watu wengi walioshuhudia kaburi hilo kuamini katika uchawi, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye alionekana ni mcha Mungu alisema hakuna uchawi wowote zaidi ya ardhi kutitia na kusababisha mmomonyoko wa udongo.
“Jamani siyo uchawi, hivi vitu vinatokea. Hapa itakuwa wakati wa kuzika, kulikuwa na uwazi umeachwa hivyo ardhi iliposhuka kuziba uwazi huo ndipo iliposababisha tobo,” alisema shuhuda huyo mcha Mungu.
Kuambiana alikutwa na umauti Mei 17, mwaka huu alipokuwa akipelekwa katika Hospitali ya Mama Ngoma, Mwenge, Dar baada ya kuugua ghafla akiwa hotelini alipokuwa amepanga kwa ajili ya kuandaa filamu.