Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol), Tawi la Tanzania, limemhoji kwa saa kumi na moja binti aliyerubuniwa na kupelekwa China ambako kwa miezi mitatu alikuwa akitumikishwa kwenye madanguro nchini humo.
Siku chache zilizopita, gazeti hili liliandika mfululizo, makala kuhusu msichana Munira Mathias, (si jina lake halisi) aliyetumikishwa kwenye madanguro nchini China, baada ya kurubuniwa kwamba alikuwa akipelekwa kufanya kazi kwenye hoteli kubwa.
Munira alisema baada ya taarifa zake kuandikwa na gazeti hili Interpol walimtaka afike ofisini kwao kwa mahojiano. Mara ya kwanza alihojiwa kwa saa saba na aliitwa tena mara ya pili na kuhojiwa kwa saa tatu na nusu.
“Walinihoji jinsi safari yangu ilivyokuwa na namna ambavyo wale wanawake waliotuchukua kutoka hapa (Tanzania) hadi China na walivyosuka mipango ya kunisafirisha,” alisema.
Alisema: “Walikuwa wanataka kuendelea kufahamu kwa kina jinsi nilivyosafirishwa na walionisafirisha, hata hivyo nimewapa ushirikiano wa kutosha.”
Mkuu wa Interpol Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile alikiri ofisi yake kumhoji Munira na kwamba lengo ni kufahamu kwa undani jinsi Watanzania wanavyotumikishwa kwenye madanguro hayo, pamoja na kujua jinsi biashara ya binadamu kati ya China na Tanzania inavyofanyika.
“Nia ilikuwa ni kujua namna wasichana wanavyotolewa hapa na kupelekwa huko, lakini kikubwa ni kufanya kazi yetu kukomesha biashara hiyo kimataifa,” alisema Babile.
Alisema siyo mara ya kwanza kwa Interpol kufanya jitihada za kukomesha biashara ya binadamu na kwamba hatua zimekuwa zikichukuliwa kila mara na siyo kwa Watanzania pekee, bali hata raia wa kigeni wanaokuja nchini.
“Tunafanya hii operesheni mara kwa mara. Kwa mfano, waliwahi kuletwa wanawake kutoka Nepal, walipofika hapa hati zao za kusafiria zikafichwa na wale wanaowatumikisha na wakaanza kufanya biashara ya ukahaba na baadaye kuwalipa wale waliowaleta,”alisema Babile.
Alisema kitengo hicho kimewahi kuwarudisha wanawake kutoka China waliofika hapa nchini kwa nia ya kufanya biashara ya ukahaba.
Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Lucy Ngonyani ambaye ndiye aliyemhoji Munira alisema wanaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio la binti huyo kupelekwa China na matukio mengine yenye uhusiano au kufanana na hilo.
dah jamani
ReplyDeletembona wengi tu wanapelekwa nchi za kiarabu wakidai wanaenda kufanya kazi za ndani kumbe ukweli ni biashara ya danguro .
ReplyDelete