Ongezeko la wasanii kushoot video kutumia waongozaji wa nje; Tobo linalovuja kwenye muziki wa Bongo

Wiki za hivi karibuni kumekuwepo na mjadala mrefu kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na wimbi la wasanii wa Tanzania kwenda kushoot video zao Kenya au Afrika Kusini au wengine kuwaleta waongozaji wa Kenya hususan Ogopa Videos, Enos Olik au Kevin Bosco Jr.


Ukweli ni kwamba hilo sio jambo la kulaumu kwakuwa msanii ana haki ya kuamua wapi, nani na lini ashoot video yake. Mara nyingi uamuzi wa kutumia muongozaji wa nje hutokana na msanii kutaka kitu kikubwa zaidi ya anachoweza kupata nyumbani na nia ya wasanii wengi wakubwa wa Tanzania kutaka kufanikiwa kimataifa pia.

Tangu wasanii kama AY, Diamond, Ommy Dimpoz na wengine kuanza kutumia waongozaji wakubwa barani Afrika, mabadiliko yameonekana kwani video hizo zimekuwa zikichezwa kwenye vituo vya runinga ambavyo huchagua sana video za kucheza. Channel O ambayo imekuwa ikizipokea baadhi ya video za waongozaji wa Tanzania, kwa sasa si kipimo tosha cha ubora wa video hizo kwani nyingi zinazokubalika hapo, zimekuwa zikishindwa kukidhi viwango vya vituo vingine kama Trace TV na MTV Base.Kwahiyo bila kuzungusha maneno, kuna tatizo katika kile waongozaji wa video wa Tanzania wanaweza kufanya.

Ongezeko la wasanii kuwatumia waongozaji wa nje ni ishara kuwa waongozaji wa ndani hawana ujuzi wa kutosha au ubunifu wa kufanya video nzuri. Tatizo ni nini? Producer Lucci amewahi kutaja sababu tatu kubwa: Vifaa, Ujuzi na Connections za waongozaji.

Hata hivyo mshindi wa tuzo za watu katika kipengele cha muongozaji wa video za muziki zinazopendwa, Nisher alipinga kuwa vifaa na ujuzi sio tatizo, na kutaja kuwa fedha wanayolipwa na wasanii ni sababu kubwa.

Nisher anaamini kuwa kama wasanii wakiwalipa fedha ya uhakika, waongozaji wa Tanzania wanao uwezo wa kufanya video zenye ubora sawa na wanazofanya waongozaji kama Sesan, Godfather, Moe Musa au Clarence Peter. Je hilo ni kweli? Hizi ni points kadhaa za wadau wa muziki walizozitoa kujadili suala hili:

Nchakalih

Msururu wa wasanii wa kibongo wanaoenda kushoot video zao nje ya tanzania ni ishara ya tatizo katika sekta hii…tusilaumiane..TUTAFUTE JIBU. Kuna artist aliniambia kwamba sababu inayompelekea kushoot nje ni ile hali ya kuchukuliana poa kati ya directors na wasanii. Naye director mmoja akasema wasanii wa nyumbani wakipewa budget kubwa wanagoma ila wako tayari kulipa bajeti kubwa na director wa nje. Wasanii wanadai madirector wa nyumbani wameishiwa mawazo mapya. ..kitu ambacho director’s wanasema kinatokana na nyimbo mbovu mbovu. Video and film production kama sekta nyingine imefika sehemu ambapo uweledi ndio kinachohitajika..na mwenye mpunga anaamua where to go. Msanii anapata kisu kirefu na halipi kodi. ..anaamua kushoot video nje ya nchi na kulipa kodi husika huko aliko. Director wa hapa nyumbani anaagiza camera’s za kisasa na kulipa ushuru mkubwa. .akitaka kushoot lazima alipie vibali husika. Ilimradi mwenye kisu kikali ndio atakula nyama. ..wasanii wataendelea kufanya wawezalo kukuza BRAND ZAO. ..collabo za nje. .videoz etc. Directors nao wagundue ushindani umeingia na kukimbilia kivuli cha bendera hakutosaidia.

Pat Nanyaro

Ishara kwamba location za tanzania bado hafifu am ndo kwamba bong utaal wa kushoot ni f ufumbuzi wa haraka un ahitajika sana. Moja ya issue ni: msanii anahisi hana ‘kiki’ kumuweka Channel O ama Trace, anatumia Director mwenye kiki….ama! Mbili…kasumba kuwa kazi ya nje ya nchi ina kiwango kuliko ya ndani, kutokana na kazi nyingi za nje kung’aa kimataifa. Ila pia tuhoji…je kila video ya nje ni mamilioni yanayotajwa? Watu fUlani walihoji “Video ya 70m unaendesha gari ya 7m?”

Fredrick Max

Sio kwenye sekta hiyo tu…watanzania wengi Pia..hawanunui bidhaa ta Tanzania…#lackofpatriotism. Kukosekana kwa uzalendo.. Hata kama bidhaa za ndani zina ubora Bado Watu watataka..kununua za nje ..it seems cool that way. Nakubaliana quality is important lakini unakuwa na quality sawa nje na ndani…ni muhimu kucreate jobs..nyumbani. Sababu nyingine ni directors wa nje tayari sana Rapport na Major channels…nyimbo kuchezwa inakuwa rahisi.

Kibanga Omar

Wasanii hawawazi vizuri, kama mtu anaulizwa na rais asaidiwe nini anasema asaidiwe afanye collabo na wasanii wakubwa. Badala ya kuwaza wananyanyuaje mziki wa nyumbani, wanajaribu kuwaza wataufunikaje muziki wa nyumbani. Kama ambavyo wasanii wanapiga hatua,video producers nao wanapiga hatua,ila wasanii wakubwa hawawapi ushirikiano mzuri. Kwanza hyo bajeti nzuri hawatoi, Nisher tayari kasema, Adam J kasema pia. na sio kweli kwamba producers hawako vizuri. Kuna video tunaziona mbaya kabisa lakini tunalazimishwa kwamba ni za bei ghali ili tuzione kali. So mi nadhani wasanii wakubwa wawaamini producers wa ndani, wasiache mbachao kwa msala upitao. Labda kama wanaenda nje ili waweze kutudanganya kwamba video hii ni ya milioni kadhaa halafu tushindwe kujua ukweli. Sababu hoja ya uzuri wa video haina mashiko, tunaona nyingi tu wanazotolea nje zinakimbizwa na zinazotolewa ndani. Watoe bajeti kubwa kwa producers wa ndani sio wadanganye danganye tu kuhusu gharama ili tuwaone expensive.

Joseph Ngowi

Sio nyingi sana maana wasanii ni wachache walioanza kushoot video nje. Bt kama amelipia hela nyingi na video ni mbovu, wehu. Video kama Come Over, Me & You na kuna ile ya Suma Mnazareti alishoot South Africa, na kuna issue ya kuongeza 0 kwenye bajeti. Hakuna tatizo kwenye hii sekta, kila mtu anataka kushoot video Dar but there is a lot of locations in this country.

Michael Baruti

Wakati Benchmark na Adam Juma wanafanya production za kweli hamna alokua anaenda nje kufanya videos.. what went wrong? Probably wasanii wako sahihi,hamna creativity tena Bongo? Directors are not pushing themselves hard enough? Kazi imekua routine. Noorah’s Ice Cream, Prof Jizze’s Zali la Mentali and all… that was pushing the limits, creativity at it’s best.. hamna now.

Nini cha kufanya?

1. Kukubali kuwa kuna tatizo

Jambo la kwanza waongozaji wa video watambue kuwa tayari kuna tatizo na wao ndio watu wa kwanza wanaotegemewa kuliondoa. Moja kwa moja hili ni jambo linalowaathiri kiuchumi sababu fedha waliyokuwa wanaipata kwa wasanii hao sasa inaenda mikononi mwa wengine. Wasanii watapunguza kuwatumia waongozaji wa nje kama tu wakihakikishiwa kuwa wale wa ndani wanaweza kuwapa video zenye ubora wanaoutafuta.

2. Wakutane kujadiliana

Waongozaji wa video nchini si wengi kiasi cha kushindwa kuandaa mkutano wao wa pamoja na kuzungumza pamoja na mambo mengine, wimbi hili. Wakutane pamoja na wajadiliane namna ya kulikabili tatizo hili.

3. Washirikiane, wasaidiane ujuzi

Waongozaji wa video Tanzania waanze kushirikiana kwa ukaribu. Wapo wengi ambao wana ujuzi wa kutosha kuwazidi wenzao. Suala la kusaidiana ujuzi kwa wengi linaweza lisiwaaingie kichwani kwa haraka, lakini kama wakiamua kuweka mbele maslahi ya sekta yao, linawezekana.

4. Waongeze ujuzi

Asilimia kubwa ya waongozaji wa video nchini wamejifunza wao wenyewe kushoot na kuhariri video. Wapo wanaotumia tutorials mtandaoni pia. Ni tofauti na waongozaji kama Moe Musa ambaye alienda chuo kikuu kusomea fani hiyo. Mtu anayefanya video kwa kutumia elimu na kipaji, huijua zaidi fani yake kuliko yule anayetumia uzoefu tu ambaye mara nyingi hufanya kwa kubahatisha. Waongozaji wafanye savings kwaajili ya kujiendeleza kielimu. Kwa wale wenye uwezo, wasafiri kwenda nchi zingine kujifunza zaidi fani hiyo. Tayari kuna taarifa kuwa muongozaji Busungu yupo/alienda nchini Afrika Kusini kuongeza elimu kuhusu masuala ya video.

5. Wafahamu kuwa wanashindana na waongozaji wa Kenya, Nigeria, Afrika Kusini na kwingine

Waongozaji wa Tanzania wanatakiwa kuwa na mawazo sawa na wasanii. Kila msanii mkubwa kwa sasa anafikiria kwenda internatioanal. Na ili uende international inabidi kuongeza wigo wa ushindani na ndio maana Diamond hashindani tena na akina Rich Mavoko, anashinda ana akina Davido. Nisher, Adam, Jerry Mushala, Nick Dizzo na waongozaji wengine waanza kushindana sasa na watu kama Moe Musa, Enos Olik, Kevin Bosco Jr, Godfather na wengine. Wakiwa na wazo hilo kichwani, watakuwa wakifanya video kwa hasira na kwa umakini zaidi.

6. Kuwekeza zaidi kwenye vifaa

Hauwezi kutengeneza video itakayokuwa na hadhi ya kimataifa kwa kutumia camera ya harusi. Video zinazofanywa na waongozaji wakubwa haziwi nzuri kimiujiza. Ni kwasababu zimefanywa kwa kutumia camera za kisasa, sets za taa zenye mwanga mzuri na vifaa vingine vya kufanyia video. Waongozaji wawe na hasira ya kukua zaidi kwa kufanya savings ili kununua vifaa bora. Wafanyabiashara wenye uchungu na muziki wa Tanzania wanaweza kuwekeza pia kwa kuagiza vifaa ambavyo wanaweza kuvifanyia biashara ya kuazima. Wapo watu wanafanya hivyo tayari lakini wanahitajika wengine wenye nguvu zaidi.

7. Watafute connections kwenye TV za nje

Sababu kubwa ya video za waongozaji wa Nigeria zinachezwa kwenye vituo vikubwa ni connections nzuri walizonazo. Waongozaji wa Tanzania wahangaike kuzipata pia, inawezekana.

8. Ni bora kufanya video chache kali kwa gharama kuliko nyingi mbaya kwa bei chee!

Baadhi ya waongozaji wa video wana kazi nyingi mno kiasi ambacho wanakosa muda wa kuelekeza ubunifu wao kwenye video husika. Ukishoot video 10 au 15 kwa mwezi mmoja, si rahisi kutoa video nzuri. Kama wakiamua kufanya video chache kwa bajeti ya kutosha (iwapo wasanii watawapa ushirikiano) tunaweza kuwa na video nyingi zenye ubora wa kimataifa.

9. Waongozaji wakubali ushauri na mawazo ya wengine

Baadhi ya waongozaji wanafahamika kuwa na tabia za ‘UMr I know Everything’ na hivyo kufanya kila wanachoona wao kipo sawa. Hakuna mtu anayejua kila kitu. Muongozaji mzuri ni yule anayemsikiliza mteja wake anataka nini na kumsaidia kumpatia kitu bora. Kuna wasanii wanadai hawawezi kufanya tena video na baadhi ya waongozaji kwa tabia zao za kuwa na ‘ego’, ujuaji mwingi na dharau.
Bongo5

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad