Askari 27 wa Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani wamefukuzwa kazi ndani ya kipindi cha miezi sita kutokana na kujihusisha na makosa ya rushwa.
Kikosi hicho ambacho kimeonya dhidi ya unyanyasaji na ushawishi wa rushwa kwa waendesha pikipiki (bodaboda), kimesema mikakati ya uchunguzi na upelelezi imeimarishwa kwa lengo la kudhibiti matukio ya rushwa miongoni mwa askari wake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Taifa, Mohamed Mpinga alisema askari hao wamekamatwa kutokana na kuimarishwa kwa usimamizi wa nidhamu na mapambano dhidi ya rushwa.
Alisema, licha ya kufanya kazi kwa weledi, upo usimamizi wa karibu kwa askari wake kwa lengo la kuepusha jeshi hilo na matukio ya aibu yakiwemo ya kujihusisha na rushwa.
“Pamoja na jitihada hizi tunaomba wananchi wote kutupa ushirikiano kupambana na hali hii hasa kwa kutoa taarifa za askari wanawaomba rushwa,” alisema Mpinga.
Alisema taarifa zitawezesha kuwashughulikia kikamilifu askari husika.
Kamanda Mpinga ameelekeza wananchi hao hususani madereva wanaoombwa rushwa na askari, kuondokana na usiri kwa kuwafichua hata baada ya kuwapatia fedha.
“Kama askari akikuomba fedha zozote ni vizuri umpatie kama unazo. Na baada ya hapo, njoo utoe taarifa kwangu nami nitakurejeshea fedha hizo,” alisisitiza Mpinga akisisitiza kwamba wanao wapelelezi wa kubaini ukweli juu ya tuhuma dhidi ya askari wao.
Akilenga kujibu malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na waendesha bodaboda dhidi ya baadhi ya askari wa usalama barabarani, Mpinga alisisitiza, “kikubwa hapa ni ushirikiano wa kila upande, utakaowezesha tabia hii kukoma.”
Mawasiliano ya karibu kamanda,maana hakuna njia traffic hachukui rushwa wanachukua wote mi niko tayari hata kutembea na kamera ya kificho,tawapa hela na picha juu!
ReplyDeleteHawa wakuu wa trafiki na maRPC ni wanafiki sana.hakuna wala rushwa wakubwa kama maRPC.hata hawa trafiki wanaonewa tu maana kimsingi wanatakiwa kupeleka hesabu kila siku jioni kwa mabosi wao na ma RPC kiasi walichokusanya kama rushwa toka barabarani.so kuwafukuza hawa ni kuwaonea tu bure na hakutamaliza tatizo.kwa taarifa ni kwamba kama trafiki hupeleki hesabu za kueleweka toka kwenye rushwa unahamishwa kituo fasta ukaongoze ng'ombe Nkasi huko.
ReplyDelete