UCHAGUZI MKUU SIMBA: Aveva apata ushindi wa kimbunga


Evans Aveva ameula baada ya kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa klabu ya Simba katika uchaguzi mkuu uliofanyika juzi kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Bwalo la Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Aveva alipata ushindi huo wa mithili ya kimbunga baada ya kupata kura 1845 na kumgaragaza mpinzani wake Andrew Tupa aliyepata kura 387 huku kura sita zikiharibika.

Katika nafasi ya Makamu wa Rais, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ameshinda nafasi hiyo baada ya kupata kura 1043 huku Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ akipata kura 413 na Swedy Mkwabi akipata kura 300.

Awali, aliyekuwa mgombea Urais wa klabu hiyo, Michael Wambura alizuiwa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba kuingia kwenye Ukumbi.

Wambura, alienguliwa kwanza kwa kuwa amesimamishwa uanachama na baadaye kwa kukiuka taratibu za uchaguzi, alishindwa kupiga kura kutokana na uamuzi wa kumzuia kuingia ukumbini.

Kwa mujibu wa wasimamizi waliokuwa wakihakiki uhalali wa wanachama kwenye uchaguzi huo, jina la Wambura halikuwapo katika orodha ya wanachama wanaostahili kupiga kura.

Wambura kama walivyokuwa wanachama wengine, walifika katika eneo la uchaguzi kwa ajili ya kukamilisha haki hiyo ya kikatiba, lakini alionekana kushangazwa na uamuzi huo wa kuzuiwa kupiga kura.

Jibu alilopewa lilimfanya kuondoka maeneo hayo kwa hasira majira ya saa 4:00 asubuhi. Wakati hayo yakitokea, wafuasi wake walionekana kukasirishwa na kitendo hicho na kutaka kufanya fujo, hata hivyo askari waliokuwapo maeneo hayo walizima jitihada hizo.

Katika mkutano huo wa uchaguzi ulioanza rasmi saa 5:00 asubuhi, lilipomalizika zoezi la wagombea kujinadi, zoezi la kupiga kura liliibua vurugu nzito kutokana na wanachama wengine kukosa karatasi za kupigia kura kwa nafasi za rais na makamu wake.

Hali hiyo ilichangiwa na wanachama kushindwa kuwa na utulivu. Hata hivyo, baada ya muda zoezi hilo liliendelea kukiwa  na utulivu mdogo katika zoezi hilo la kupiga kura lililoanza saa 9:00 alasiri na kura kuhesabiwa saa 11:00 jioni.
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. mi nashangaa tufikie wakati tuwe kama wenzetu wa ughaibuni kujiuzuru kama watu hawakuhitaji au mpaka utolewe roho wambura nini kama kula ushakula sana na hakuna mabadiliko watu wanataka mabadiliko sasa

    ReplyDelete
  2. template ya blog ni mbaya,,,, rudisha ilokuepo zaman

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad