Walio Tupa Viungo Vya Binadamu Bunju Wapandishwa Kizimbani, Mashataka Yafutwa

Sakata la kutupwa kwa viungo vya binadamu bila kufuata utaratibu jana liligeuka sinema wakati maofisa wanne wa Chuo Kikuu cha Tiba na Teknolojia (IMTU), walipofikishwa mahakamani Dar es Salaam.

Maofisa hao ambao ni maprofesa na wahadhiri wa chuo hicho walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kushindwa kufukia viroba 83 vya miili ya binadamu.

Baada ya mashtaka hayo kusomwa na taratibu za dhamana kukamilika huku mmoja wao akishindwa kutimiza masharti, watuhumiwa hao walirejeshwa kizimbani na kufutiwa mashtaka hayo kwa amri ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP) aliyewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka hayo.

Hata hivyo, furaha waliyoipata washtakiwa hao, Venkat Subbaiah (57), Appm Shankar Rao (64), Prabhakar  Rai (69) na Dinesh Kumar (27) ilikuwa ya muda tu, kwani polisi waliokuwapo mahakamani hapo waliwakamata tena na kuondoka nao.

Mashtaka yafutwa

Wakati washtakiwa hao wakikamilisha taratibu za dhamana wakiwa ndani ya mahakama hiyo, Wakili wa Serikali, Salum Ahmed aliingia na kuiomba mahakama kuifuta kesi hiyo chini ya Kifungu cha 91 (1) cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi yao.

Kifungu hicho cha sheria kinampa mamlaka DPP kuifuta kesi mahakamani wakati wowote pale anapoona hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi ya mtu yoyote.

Baada ya kuwasilishwa kwa ombi hilo, Hakimu Rusemwa aliwaachia huru washtakiwa hao bila masharti yoyote.

Wakamatwa tena

Muda mfupi baada ya washtakiwa hao kuwa huru, walianza kutoka mahakamani kwa furaha lakini kumbe furaha yenyewe ilikuwa inaishia mlangoni mwa mahakama hiyo tu kwani walikutana na polisi waliowakamata tena na kuwaweka chini ya ulinzi.

Wakati washtakiwa hao wakiwa chini ya ulinzi, Wakili wao, Gaudiosus Ishengoma alieleza kusikitishwa na kitendo hicho, akidai DPP aliwafutia mashtaka wateja wake na kuwaachia huru ili awafungulie mashtaka mengine ambayo hayana dhamana.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad