Kufuru:Bunge Lakodi Vipaza Sauti kwa Sh8.9 Milioni Kila Siku

Wakati kukiwa na malalamiko kwamba Bunge la Maalumu la Katiba linagharimu fedha nyingi za walipakodi, uongozi wa taasisi hiyo umetumia Sh142.56 milioni kukodi vipaza sauti kutoka Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alithibitisha kukodiwa kwa vipaza sauti hivyo kwa ajili kamati zote 12 na kwamba kila gharama ya chumba kimoja kwa siku ni Dola 450 za Marekani (Dola moja ni wastani wa Sh1,650).

Kwa maana hiyo Bunge, hilo linatumia Dola 5,400 sawa na Sh8.91 milioni kwa siku kugharimia vipaza sauti katika vyumba 12 vinavyotumiwa na kamati hizo na kwa siku 16  ambazo kamati zitakutana, gharama hizo zitafikia Sh142.56.

“Vifaa vya sauti tulivyokuwa navyo vinalalamikiwa, vilikuwa siyo standard (viwango) hasa vya mazungumzo, tumekodi kutoka Ukumbi wa Mikutano wa AICC na tumekuwa nao usiku mzima kuvifunga,” alisema.

Alisema tangu wavifunge, hawajawahi kupata malalamiko tena kutoka katika kamati kuhusu ubora na kwamba gharama za kukodisha vifaa hivyo itatoka katika fungu la dharura la Bunge Maalumu.

“Mara ya kwanza walituambia gharama zao ni Dola 500 kwa siku lakini tukajadiliana nao, hivyo tukafikia kiwango hicho cha Dola 450,” alisema.

Hamad alisema vifaa vya awali ambavyo vililalamikiwa na wajumbe kuwa havitoshi, vinatoa sauti nje ya majengo na kwa jinsi vilivyo, vinalazimika kutembezwa ukumbini, hivyo kusababisha usumbufu.

Malalamiko ya gharama

Suala la gharama limekuwa likiibuka mara kwa mara na wakati mwingine kutajwa kama sababu ya kuahirishwa kwa Bunge hilo kwa kuwa hakuna uhakika wa kupatikana kwa akidi inayotakiwa kufikia uamuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alilalamikia kile alichokiita “matumizi ya kufuru” ya Bunge Maalumu wakati hakuna uhakika wa kupatikana kwa Katiba Mpya.

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad