Kumbe Manyaunyau ni Tapeli: Shahidi Aelezea Jinsi Walivyotapeliwa Sh 29.6 Mil na Mganga Huyo

Dar es Salaam, Shahidi wa pili katika kesi ya kujipatia Sh29.6 milioni kwa njia ya udanganyifu inayomkabili mganga wa jadi, Dunia Salumu (37) ‘Manyaunyau’ amedai kuwa walilazimika kuuza kiwanja na nyumba ya urithi kutafuta fedha za kununua mabeberu saba na mafuta ya ngamia ili kumpa mganga huyo kama masharti ya kumfufua ndugu yao aliyefariki dunia.

Manyaunyau alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Desemba mwaka 2013 akikabiliwa na shtaka la kujipatia fedha hizo kutoka kwa Tecla Modest.

Akiongozwa na Mwendesha Mashtaka, Nassoro Katuda shahidi huyo, Diana Steven (26) alidai kuwa baada ya kumaliza matanga ya mjomba wake, Saimon Modest aliyefariki mwaka 2008, wakiwa nyumbani Mchikichini, Dar es Salaam walisikia sauti ya mtu ikisema kuwa ‘mimi sijafa’.

Wakati Diana akiendelea kutoa ushahidi huo mrefu, Hakimu Wilberforce Luhwago, alimkatisha akieleza kuwa ameisikiliza kesi hiyo kwa muda mrefu na kuna nyingine za kusikiliza, hivyo itaendelea Agosti 13, mwaka huu.

Ushahidi wenyewe

Alisema siku tatu baada ya mazishi ya mjomba wake, ndugu yao aitwaye Hamisi akiwa na Manyaunyau walifika nyumbani kutoa pole na walipofika Manyaunyau alidai kuwa marehemu hajafa, bali ameuawa na kaka yake na amechukuliwa na Mpemba kwa ajili ya kwenda kuuza duka.

“Mimi na mama zangu wawili tulishtushwa na kuhoji, mtu aliyekufa anaweza akawa hai?” alisema Diana katika ushahidi wake uliochukua saa nane.

“Baada ya hapo alituambia siku iliyofuata twende ofisini kwake (Manyaunyau), Mburahati, tukiwa na Sh100,000. Mama zangu walisema hawana, lakini ndugu yetu mmoja aitwaye Bright Steven alikwenda kwenye ATM na kuchukua Sh80,000 na safari ikafanikiwa,” alidai.

Diana alisema baada ya kupeleka fedha hizo, Manyaunyau aliwapangia kwenda siku nyingine, akiwataka kurudi wakiwa na kitambaa cheusi na walipokipeleka alisema alikichukua na kukifunika kikaanza kutoa sauti ya mtu mzima ikisema: “Karibuni sana wajukuu zangu na maelezo yote mtapewa na mwenyeji wenu.”

Alisema Manyaunyau pia aliwataka wapeleke chupa sita za mafuta ya ngamia wakiyakosa wampelekee Sh1.8 milioni. Alisema walimpelekea fedha hizo walizozipata kwa kuuza sehemu ya kiwanja walichorithi kwa mama yao.

“Siku tuliyopeleka hiyo hela pia tulipeleka mtama, jogoo mwekundu na tulipelekwa katika pori lililopo Kibamba na kila tulipokuwa tukienda kule Kibamba tulikuwa tunakodi teksi kwa Sh40,000,” alidai Diana.

Alidai kuwa kabla ya kufika katika pori hilo, Manyaunyau aliwaagizia soda wakanywa na baada ya kumaliza aliwaambia wapige makofi huku wakisema hodi hodi mkubwa!

“Tuliingia katika pori hilo saa 2: 00 usiku, tukaona mwanga kama radi imepiga na tukaona kitu cheupe kama mtu kafunikwa sanda... ile tuliyoipeleka kwa Manyaunyau siku chache kabla ya kwenda katika pori hilo.

“Alituambia mtu wenu ndiyo huyo ila msimfunue kwa sababu ni mchafu, akasema inatakiwa hela ya kununua mafungu mawili ya dawa ya kumsafishia.

Sisi hatukuelewa, ndipo alipotuambia siku iliyofuata twende ofisini kwake atufafanulie. Tulipofika alituambia anataka mbuzi saba madume na Sh2 milioni na kwenda naye tena Kibamba.

“Tukiwa porini hapo tulisikia sauti ya babu ikisema marehemu wenu ameshikiliwa na wachawi, wanataka damu ya mbuzi saba, hivyo tulirudi nyumbani na kwenda kuuza tena kiwanja kilekile kwa mtu mwingine na kupata Sh4.9 milioni na kuzipeleka kwa Manyaunyau kununulia mbuzi hao,” shahidi alidai na kuongeza kuwa ‘babu’ alizidi kuongeza madai, mara hii akisema anataka nguo, mkeka na chakula nyumbani kwa Manyaunyau.

“Baada ya kauli ya babu, tulipeleka chakula kwa Manyaunyau na hapo alituambia tujiandae kwa safari ya Majohe na huko tulikwenda mimi na mama zangu wawili na mke wa Manyaunyau na tulipofika tuliongea tena na ‘babu’ na kutuambia tutafute Sh2 milioni nyingine kwa ajili ya kumkomboa ndugu yetu.”

Waliporudi kutoka Majohe, alidai kuwa walikwenda kukopa kwa riba na Manyaunyau alisema fedha hizo wazifunge katika kitambaa cheusi na kuziweka katika ndoo na kuzipeleka katika Msitu wa Majohe.

“Tulipofika Majohe tulipiga makofi na kuziweka zile pesa na siku iliyofuata Manyaunyau alituambia tutoe Sh3.5 milioni kwa ajili ya kukanyagia na sisi tulizipelekea hukohuko Majohe.”

Alidai kuwa siku iliyofuata walikwenda ofisini kwa Manyaunyau na kuambiwa kuwa wapeleke chakula nyumbani kwake baada ya hapo waende kumwangalia mchawi aliyemchukua ndugu yao huko Kibamba eneo la makaburi.

“Tulipofika eneo hilo la makaburi alitokea mtu mrefu sana akiwa ameshikilia mkia na akapiga magoti na hapo hapo alitokea tena mtu mnene na kusema hamuwezi kumuona ndugu yenu kwa sasa.”

Diana alidai kuwa baada ya kuambiwa hivyo, ilisikika sauti ya ‘babu’ ikisema watafute Sh5 milioni nyingine.

“Tulivyosikia hiyo sauti ya ‘babu’ akisema tutafute ndugu zangu walisema hawana hiyo hela na sauti ya babu iliendelea kusema kuwa nyie leteni tu hiyo hela marehemu akija atailipa,” alieleza.

Post a Comment

6 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Jtano mie ilalaaaa,muvi tamu balaa

    ReplyDelete
  2. ama kweli nyie wendawazimu hivi toka mzaliwe mpaka mmekuwa wakubwa katika kizazi hiki mlisikia wapi kuna mtu kaweza kumfufua mfu?....Wajinga ndio waliowao mkome siku nyingine kuendekeza ushirikina

    ReplyDelete
  3. Nyie familia nzima hamna dini?..wala hamjui Muumba wenu ni nani?...kama kweli huyo manyaunyau ni mfufuaji wafu hata kama anaouwezo wa kuwarudish wale msikule...basi angekuwa mbali..maana hicho ni kipaji kutoka kwa Mwenyezi Mungu.kama alivyowajaalia mitume wake kama Yesu n.k....lakini sio huyo mwanga,mshirikina manyaunyau...Hizo pesa zenu hata kama amebaki na nusu awarudishieni au afirisiwe mali zake..nakueleweni pengine aliwapumbaza kwanza ndo akaanza kuwachuna namna hiyo..Sasa hilo ni fundisho kwa yeyote aendae kwa mganga na Akome,kwani huwa wanakupakeni chuma ulete..hutaweza kuishi bila mganga..na kumbukeni kw Mola mna adhabu kali mno...Mola Atusamehe

    ReplyDelete
  4. Huyu mheshmiwa manyaunyau kajua kuzitafuna hela za hawa bandugu... hata huruma hana, daaah hii kiboko. Ila me cwalaumu ujue mtu unapokua na shida unajikuta unafanya mambo hukuwai dhani ka utaja fanya.. walotaka mrudisha mjomba wao kipenzi!!!

    ReplyDelete
  5. JAMANI TAPELI HANA HURUMA JAMANI ANAHAKIKISHA UMEISHIWA MPAKA TONE LA MWISHO ,UNAONGEA PEKE YAKO NJIANI KAMA MWENDAWAZIMU NDO ANAKUACHIA, WPO WATU WLIKUWA MATAJIRI LAKINI WAKUKUTANA NA MATAPELI WAKAFANYA KAZI ZAO KWISHINEY WANACHOMA MAHINDI TU SASA

    ReplyDelete
  6. FAMILIA HII ILISHINDWA KUJUA UKWELI KUHUSU MTU AKIFAA, SASA WAKIAMBIWA WAMJUE MUNGU HAWATAKI, HELA LAZIMA ZIWATOKE.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad