Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa anataka na anatamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania kuongoza nchi ambayo ni maskini na hivyo atatumia muda wake uliobakia katika uongozi kuelekeza nchi kwenye mwelekeo huo.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa jambo la msingi kabisa la kama Watanzania watanufaika na ugunduzi wa gesi asili ama watabakia katika hali yao ya sasa ya umasikini ni aina ya uongozi ambao nchi hiyo itaupata, uongozi wenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa kadri nchi inavyozidi kusonga mbele.
Rais Kikwete pia anasema kuwa Tanzania inatarajia kuanza kupokea mapato yake ya kwanza kutokana na raslimali ya gesi asilia katika miaka sita ijayo, kuanzia Mwaka 2020.
Rais Kikwete ameyasema hayo jana, Jumatatu, Agosti 4, 2014, wakati alipozungumza kwenye Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo (Centre for Global Development) mjini Washington,D.C., Marekani, ambako alizungumzia Hali ya Baadaye ya Tanzania kufuatia Ugunduzi wa Gesi – Future of Tanzania following the Discoveries of Gas.
Rais Kikwete yuko nchini Marekani kwa ziara rasmi ya siku tisa ambako miongoni mwa mambo mengine atahudhuria Mkutano wa Kwanza wa Viongozi wa Marekani na Afrika ulioitishwa na Rais Barack Obama wa Marekani na unaoanza leo, Jumanne, Agosti 5, 2014.
Rais Kikwete ameuambia mkutano kwenye Kituo hicho kuwa anataka kufanya kila linalowezekana katika kipindi chake kilichobakia cha uongozi kuhakikisha kuwa anaanzisha na kuanza kujenga taasisi na kuweka kanuni sahihi za kuweza kusimamia raslimali ya gesi asilia .
“Nitafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa Watanzania na nchi yao wananufaika kutokana na mapato ya raslimali kutokana na gesi asilia. Nataka na natamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania kuongoza nchi masikini. Raslimali ya gesi inatoa nafasi na fursa kubwa kwa nchi yetu kuondokana na umasikini. Mimi nimeongoza nchi masikini, lakini nataka mrithi wangu kuongoza nchi yenye ustawi na utajiri,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Hivyo, dhamira na shughuli yangu kubwa kati ya sasa na mwisho wa kipindi changu cha uongozi ni kuiongoza nchi yetu kuelekea kwenye njia hiyo ambako gesi italeta ustawi na utajiri na maisha bora zaidi kwa wananchi wetu.”
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa ili Watanzania wanufaike na mapato ya gesi ni muhimu kuwepo na uongozi imara ambao utakuwa tayari kuchukua maamuzi sahihi kwa kadri nchi inavyosonga mbele. “Jambo la kutia moyo ni kwamba Tanzania ni demokrasia, na ushiriki wa umma kutaja kujua nini kinaendelea uko juu sana.”
Tanzania imekuwa inatafuta gesi na mafuta tokea miaka ya 1950 na ugunduzi wa kwanza ulikuwa Mwaka 1974 katika Kisiwa cha Songo Songo kilichoko Mkoa wa Lindi na Mnazi Bay katika Mkoa wa Mtwara mwaka 1982.
Hata hivyo, ilikuwa kuanzia Mwaka 2010 wakati ugunduzi mkubwa wa gesi ulipofanyika kwenye eneo la bahari, ugunduzi ambao mpaka sasa umefikia futi za ujazo trilioni 50.5.