SIKU moja baada ya Mbunge wa Maswa Magharibi, mkoani Simiyu, Bw. John Shibuda kutangaza kuachia ngazi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mbunge huyo ameibuka tena na kusema aliahidiwa kupewa helikopta mbili na uongozi wa chama hicho aweze kuzitumia katika kampeni za Uchaguzi Mkuu 2010 lakini hakupewa.
Alisema uongozi wa chama hicho ukiongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Wilbrod Slaa, ulimwahidi kumpa helikopta hizo kwenye kampeni zake na kumpigia debe Katibu huyo aliyekuwa akiwania nafasi ya urais.
Bw. Shibuda aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Malampaka, wilayani Maswa na kuongeza kuwa, alijitolea kutumia pesa zake katika uchaguzi huo na kuahidiwa kurudishiwa lakini mpaka sasa bado kurudishwa.
“Katika kampeni za mwaka 2010, mbali ya kuahidiwa helikopta, pia nilikuwa chanzo kikubwa cha Dkt. Slaa kupata kura nyingi kwa mara ya kwanza na kuongoza kwenye Wilaya ya Maswa akimzidi mgombea mwenzake kutoka CCM, Rais Jakaya Kikwete.
“Helikopta nilizoahidiwa, hata wakati wa kampeni sikupewa, nilipouliza niliambiwa nitapewa…mimi ndiye chanzo kikubwa cha Rais Kikwete kupata kura ndogo katika jimbo langu, nilitumia gharama zangu kumfanyia kampeni Dkt. Slaa,” alisema.
Wakati huo huo, Bw. Shibuda alisema msimamo wake ni Serikali mbili na kusisitiza hawezi kuwaunga mkono wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao msimamo wao ni Serikali tatu ambazo zitawaongezea mzigo wananchi wangu ambao ni wakulima na wafugaji.
Bw. Shibuda alisema wananchi wake hawataki kuongezewa mzigo wa Serikali; bali wanataka kutatuliwa kero walizonazo hasa zinazohusu kilimo cha pamba, migogoro ya wakulima na wafugaji.
“Siko tayari kuunga mkono muundo wa Serikali tatu kwa sababu wakulima wa pamba wana matatizo makubwa katika bei ya zao hili na pembejeo, pia katika wilaya yangu kuna migogoro mikubwa ya wakulima na wafugaji inayopaswa kutatuliwa kwa serikali hii tuliyonayo,” alisema Bw. Shibuda.
Katika mkutano huo, Bw. Shibuda alikwenda mbali zaidi akimfananisha Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni Mwanasheria wa chama hicho, Bw. Tundu Lissu na kundi la Interahamwe lililochochea ubaguzi wa kikabila uliosababisha mauaji ya kimbari nchini Rwanda akidai mbunge huyo amekuwa mchochezi wa vita ndani na nje ya chama.
“Tundu Lissu ni Interahamwe kwani amekuwa mtu mchochezi mwenye tabia ya kuwatukana wenzake, hana tofauti na kundi hili kama wenzake walivyosababisha mauaji nchini Rwanda,” alisema.
Credit: Majira
njaa mbaya, kwani shibuda una kazi gani zaidi ya ubunge, lakini tatu nyingi sana aisee lazima ulopoke
ReplyDeleteyote hiyo ni njaa wamenyimwa ugali pole kaka
ReplyDeletekiongozi ni mtu anayejitolea kwa hali na mali, sasa wewe kutumia hela yako imekuwa nongwa? na hata hivo hizo pesa ulikua unahonga au?
ReplyDeleteShibuda CCM Mtu yyo kutoka CCM lazima atakataa Serikali tatu kwa sababu wanajua Tanganyika walikoiuza, ndio maana migogoro ya Ardhi Tanganyika haiishi kwa sababu ilishauzwa zamani sana
ReplyDeleteinabidi apeleke ushibuda wake huko alikotoka na kukaa kimyaaa!!!! njaaa tu inamsumbua huyu
ReplyDeleteTanzania hakuna mwanasiasa mzalendo wa kweli hata 1 wapumbavu endeleeni kushabikia vyama na maigizo yao badala ya kufanya kaz
ReplyDeleteutakuwa bwege kama utakaa na kushabikia vyama nakuacha kupiga kazi, sababu sidhani kama kuna mtu yeyote mwenye akili timamu anayesubiri chama fulani kimpe maisha, ila tu tunachokipigania ni kile chama ambacho kimekaa madarakani kwa miongo mingi na bila kuleta tija na manafuaa kwa watu wengi, kama wameshindwa wakae pembeni tuwaone wengine nao wajaribu, nao wakishindwa basi nao watakaa pembeni, huo ndiyo mtazamo wangu, siyo unanangania tuuuu sababu ya tumbo lako!
ReplyDelete