Tume ya Warioba Yaivua Nguo Serikali Hadharani Katika Mdahalo

JANA taifa lilisimama saa nne kwa Watanzania kuelekeza masikio na macho kwenye runinga kusikiliza ufafanuzi wa wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, juu ya upotoshaji wa viongozi waandamizi wa serikali kuhusu mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu ya katiba mpya.

Wajumbe wa yume hiyo wakiongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba, waliwataja viongozi hao kuwa ni Stephen Wassira, William Lukuvi, Anna Tibaijuka na Mwigulu Nchemba katika mdahalo wa katiba mpya uliofanyika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, uliondaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na kurushwa na runinga ya ITV.

Jaji Warioba, alianza kwa kuweka hadharani namna watu wenye propaganda za mfumo wa serikali mbili wanavyopotosha maana nzima ya rasimu ya pili ya tume hiyo inayoelekeza mfumo wa serikali tatu.

Alisema watetezi wa serikali mbili, wamejikita kuelezea upungufu wa serikali tatu huku wakiacha mazuri ya muundo huo pamoja na udhaifu wa serikali mbili za sasa.

Jaji Warioba, alikanusha kauli iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Bunge, William Lukuvi, kuwa kuna maoni mapya yamewasilishwa serikalini.

Alisema hajabadilika katika msimamo wake wa kutetea serikali tatu kama wananchi walivyotaka, na kwamba kinachofanywa na wanaoeneza maneno hayo ni uzushi wenye malengo maalum.

Alifafanua kuwa kilichofanywa na wao ni kupeleka serikalini yale mambo ambayo waliyachuja na ambayo yasingekuwa na nafasi katika Serikali ya Muungano zaidi ya kusubiri Katiba ya Tanganyika.

“Sijabadilika, na jambo la msingi ni kwamba yale tuliyoyachuja badala ya kutupa tulisema tukakabidhi serikalini kwa ajili ya kusaidia kuwa kumbukumbu kwao pale watakapoona wanakwama, lakini muhimu hayo wanayosema tumepeleka kuonyesha kuwa tumebadilika ni vema waweke hadharani,” alisema Jaji Warioba.

Alisema bado kuna haja ya viongozi kuendelea kuvumiliana na kutafuta maridhiano yatakayozaa katiba bora ya Watanzania, huku akibainisha kuwa hata wao walikuwa na tofauti zilizomalizwa kwa kuangalia maslahi ya taifa badala ya makundi waliyotoka.

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. hayo siku hizi hayaangalii maslahi ya taifa, yanaangalia maslahi ya matumbo yao tu!

    ReplyDelete
  2. si kwamba anatingisha kiberiti pia kuhusu kukubalika likubaliwe nanani kwasababu serikali ilioko madarakani ndio inakataa lakini wananchi wamependekeza kwahiyo serikali itoe sababu za kuridhisha wananchi waliopendekeza serikali tatu sio waseme juju tu wawaelimishe kwanza hasara yake na faida ili waelewe sababu

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad