CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimebaini njama ya serikali za kutaka kununua helikopta tatu nchini China kwa ajili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku wakidai kuwa ni mali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Pia kimesema kinaanza ziara ya makundi nchi nzima ili kuwahamasisha watanzania kuikataa Katiba inayopendekezwa kwa madai imechakachuliwa kwa manufaa ya vigogo wa CCM.
Hayo yamebainishwa jana na Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk. Willibrod Slaa wakati akitoa maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho kuhusu mchakato wa Katiba na hatua ya kuipigia kura maoni Katiba inayopendekezwa.
Katika mkutano huo, Dk. Slaa alisema ana taarifa za uhakika kwamba mchakato wa ununuzi wa Chopa hizo tatu, utakamilishwa wakati wa ziara ya Rais Kikwete anayetarajia kuzuru nchi hiyo hivi karibuni.
Katibu Mkuu huyo alisema taarifa alizonazo ni kwamba Chopa hizo zinataka kununuliwa na Rais Kikwete kwa ajili ya kampeni za mgombea urais wa CCM mwakani.
Alisema tayari mkakati unaopangwa na Rais Kikwete umebainika na kwamba hautakubaliwa kwa sababu haujafuata taratibu za sheria za manunuzi nchini.
“Tumebaini mkakati wa wizi wa fedha za walipakodi unaotaka kufanywa na Rais Kikwete …hatutakubali kuona fedha zao zinaliwa na mafisadi huku wakilisingizia jeshi la ulinzi nchini,” alisema Dk. Slaa
Pamoja na hilo, alisema wataendelea kufuatilia na kutoa taarifa kwa umma kwani anayeshughulika na mchakato huo, naye ni fisadi.
Bila kumtaja mhusika wa mchakato huo, Dk. Slaa alisema kilichowashtua hata kufuatilia kwa makini mkakati huo ni mhusika mkuu wa mchakato huo kuwa ni fisadi na unaweza kufanya ufisadi kama ule wa ununuzi wa Rada.
Chanzo: Tanzania daima
Chanzo: Tanzania daima