Kiungo wa AC Milan, Michael Essien amezushiwa kuwa ameambukizwa virusi vya ugonjwa hatari wa ebola.
Hali hiyo imetokana na yeye kuachwa kwenye kikosi cha timu yake ya taifa ya Ghana, Black Star ambacho kilicheza mechi ya mwisho ya kuwania kucheza Kombe la Mataifa Afrika na kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Guinea.
Hivyo habari zikazagaa kwenye mitandao mbalimbali ikiwemo ya kijamii, kwamba anaugua.
Lakini Essien amekanusha vikali hali hiyo kupitia mitandao ya kijamii na kusema si jambo zuri kulifanyia utani.
“Mimi niko fiti kimwili, kiliakili. Kesho nitaendelea na mazoezi na AC Milan kama kawaida,” aliandika kiungo huyo wa zamani wa Chelsea na Real Madrid.
“Ebola ni jambo baya na tunahitaji kuwasaidia waathirika na si vema kulitumia kama sehemu ya utani.”