Dar es Salaam. Iko dhana kuwa ili Tanzania ipige hatua kimaendeleo inahitaji kiongozi anayethubutu kufanya uamuzi mgumu hasa kuwawajibisha viongozi wabadhirifu na wazembe, lakini Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba amekwenda mbali zaidi; anasema dawa ni kufanya uamuzi wa kidikteta.
Makamba alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumamosi, ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Mbunge huyo ambaye hivi karibuni alitangaza nia ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, ametoa kauli hiyo wakati nchi ikijiandaa kwa uchaguzi huo huku tayari watu mbalimbali, hasa kutoka chama tawala cha CCM wakiwa wameshaanza kujinadi.
“Moja ya vitu vitakavyozuia rushwa ni adhabu kali ambayo itaonekana. Kwa nini madikteta wanawaua watu hadharani? Wanachojaribu kukionyesha ni kwamba kama siku moja mtu akijaribu kuwapindua atapelekwa uwanjani na kupigwa risasi hadharani. Lengo ni kuwatia watu hofu,” alisema.
Alisema, “Moja ya namna ya kupambana na rushwa ni kuwatia watu hofu, kwamba ukikamatwa yatakayokukuta ni kama yanayowakuta wenzako.”
Alisema ili kupambana na rushwa ni lazima kuwekwe mbinu za kivita na kwamba kama hilo lisipofanyika ni sawa na kupoteza muda.
“Serikali itakuwa inakusanya mapato na kupanga mambo yake, lakini asilimia 50 ya mambo hayo yanarudi mikononi mwa watu,” alisema.
Makamba alisema mmomonyoko wa maadili ni moja ya sababu inayofanya nchi ichelewe kupata maendeleo.
“Kuna wizi na ubadhilifu mkubwa siyo tu kwa viongozi wa kisiasa, hasa kwa watendaji na watumishi wa kada za kati na chini. Watu wanawatizama wabunge na waziri pekee wakati wapo wahasibu wa wizara na halmashauri,” alisema.