Kampeni za Urais CCM: Noti Zamwagwa Nec Dodoma

Baadhi ya makada wa wa CCM wanaotajwa kuwania urais kupitia chama hicho wanadaiwa kugeuza mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec), kuwa sehemu ya kampeni kwa wajumbe wa mkutano huo wakidaiwa kumwaga fedha usiku kucha.

Gazeti hili lilishuhudia kampeni hizo zikifanywa na wapambe wa wagombea hao nje ya Ukumbi wa Nec uliopo nje ya jengo la White House mjini Dodoma na baadhi ya watu wanaotajwa kuwania nafasi hiyo.

Wapambe hao kwa siku mbili za vikao vya Nec vilivyofanyika mjini hapa kuanzia juzi walionekana wakifika mapema, kusalimia, kujitenga katika makundi madogomadogo na wajumbe wa Nec tofauti na vikao vingine vilivyotangulia.

Harakati hizo hazikuishia katika viwanja hivyo, bali hata nje ambapo mmoja wa makada anayetajwa kuwania nafasi hiyo kutoka Kanda ya Ziwa ameonekana kukutana na makatibu wa CCM katika moja ya hoteli mjini hapa.

“Huyu jamaa amekutana na makatibu wa CCM mara nyingi katika kile kinachoelezwa kuwa ni kusaka wajumbe ili wasijiunge na kambi nyingine,” kilieleza chanzo chetu.

Alipoulizwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema bado hajazipata taarifa hizo na kwamba kama kuna vitendo vya rushwa vinafanyika ni nje ya mazingira hayo.

Alisema katika mazingira kunapofanyika kikao cha Nec, si rahisi kuwapo vitendo hivyo.

“Sasa kama wanapeana barabarani mimi itakuwa ni vigumu sana. Mimi ninashughulikia na mambo ya humu ndani (kikao cha Nec),”alisema na kuongeza:

“Leteni taarifa nilikuta fulani anagawa ama fulani anapokea, haya maneno ya jumla hivi yanaweza kuwa ni mkakati wa kupaka chama matope,” alisema.

Alisema kama inagawiwa usiku wakati yeye akiwa amelala hawezi kufahamu.

Makatibu na wenyeviti wa CCM wa wilaya wanaingia katika Nec kwa mujibu wa vyeo vyao.

Tayari hali hiyo imelalamikiwa na baadhi ya wajumbe wa Nec, wakisema inakitia aibu chama.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad