Utata umezidi kugubika kura mbili zilizowezesha kupitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa ambayo wiki iliyopita ilikabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein mjini Dodoma.
Utata huo unatokana na kura za wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) upande wa visiwani, wajumbe waliokuwa Hijja, Saudi Arabia na zile za baadhi ya wajumbe wanaodaiwa kuhamishwa kinyemela kutoka Bara kwenda Zanzibar au kinyume chake.
Utata Saudia
Chanzo chetu kutoka Dodoma kilisema: “Kuna utata maana hakuna uhakika iwapo kweli mahujaji ambao ni wajumbe wa Bunge la Katiba walipiga kura maana kuna barua ilitoka ubalozini Saudi Arabia ikisema hilo lisingewezekana.”
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Ubalozi wa Tanzania Riyadh, uliandika barua kwa Bunge Maalumu la Katiba ukieleza kwamba usingeweza kuratibu upigaji kura kutokana na mazingira halisi ya ibada ya Hijja.
Miongoni mwa sababu zilizotolewa na ofisi ya ubalozi huo ni kwamba mtu yeyote ambaye si hujaji hakuwa anaruhusiwa kuingia katika maeneo ya Hijja na Serikali ya Saudi Arabia ilikuwa imetoa vitambulisho maalumu kwa mahujaji tu.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alikiri kupokea barua kutoka Ubalozi wa Tanzania uliopo Riyadh, ukieleza kwamba mazingira yasingeruhusu wajumbe hao wanane kupiga kura, lakini akasema walitumia njia nyingine kufanikisha kazi hiyo.
“Tulipokea barua hiyo kweli na pengine niseme tu siyo moja, zilikuwa barua kama tatu au nne hivi, maana hata hapa foreign (Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa) Dar es Salaam walituandikia kuhusu ugumu wanaouona, lakini baada ya kuona hivyo tuliamua kutumia njia zetu wenyewe.
“Tulimtuma ofisa wetu kwenda Saudi Arabia na tulimkatia tiketi na kusema kweli wakati wote alikuwa akiwasiliana nasi, nakumbuka mtu wa kwanza kupiga kura alikuwa Raza (Mohamed, Mwakilishi wa Uzini) ambaye alikuwa Dubai na baada ya hapo alikwenda walikokuwa mahujaji wengine na walifanikisha vizuri sana,” alisema.
Wajumbe wengine waliokuwa Uarabuni kwa mujibu wa orodha iliyotangazwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta ni pamoja na Dk Abdallah Kigoda, Sheikh Mussa Kundecha, Hamza Mustapha Njozi, Dk Maua Daftari, Shawana Bukheti Hassan, Asha Mtwangi, Amina Andrew Clement na Riziki Lulida.
UJINGA MAWAKALA WALIKUWEPO MECHI IMEISHA SHIDA HATUNA LINGINE LA KUJADILI
ReplyDelete