Lowassa Aliangukia Kanisa Katoliki: Asema Maneno ya Sitta Bungeni Yapuuzwe

Wakati Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba (MBK) ikitarajia kuingia katika hatua ya kura ya maoni mwakani, Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, ameibuka na kuliomba radhi Kanisa Katoliki kufuatia mgongano iliyojitokeza kati ya kanisa hilo na baadhi ya viongozi serikali na wa Bunge hilo.

Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, aliomba msamaha huo wakati akitoa salamu zake katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Kanisa Katoliki Jimbo la Mahenge, mkoani Morogoro.

Alisema Kanisa Katoliki lina mchango mkubwa katika kudumisha amani na mshikamano nchini, hivyo mambo yaliyojitokeza yanapaswa kusamehewa.

“Najua hivi karibuni tumewaudhi, lakini mimi naomba mtusamehe bure tu, kama vile mzazi anavyomsamehe mtoto wake anapokosea,” alisema Lowassa na kuongeza kuwa Kanisa Katoliki ni muhimu katika maendeleo ya nchi.

Ingawa Lowassa hakueleza kwa undani tofauti zilizojitokeza kati ya Kanisa hilo na baadhi ya viongozi wa serikali, lakini wakati BMK likiendelea, taasisi za dini zilisambaza waraka uliosainiwa na viongozi wake ukilikosoa Bunge hilo kwa mambo mbalimbali ikiwamo kuendelea kujadili rasimu bila maridhiano kutokana na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia.

Kadhalika, viongozi wa madhahebu hayo ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Baraza la Kikiristo Tanzania (CCT) na Makanisa ya Pentekoste Tanzania (PCT), walilikosoa BMK kwa kupuuza maoni ya wananchi yaliyokuwa katika Rasimu iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Waraka huo ulisababisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, kujiweka katika wakati mgumu kwa kuzua mgogoro dhidi ya viongozi wa dini ya Kikristo, baada ya kuita waraka huo kuwa ni wa kipuuzi na wa hovyo hovyo.

Sitta ambaye alitoa kauli hiyo Oktoba Mosi mwaka huu, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa waraka wa maaskofu una lugha ya Ukawa, ingawa maaskofu kwa upande wao waliueleza kuwa ni waraka wa kinabii, kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad