Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema Rais Jakaya Kikwete haeleweki kwa sababu mambo mengi wanayokubaliana naye anayafanya kinyume.
Akizungumza Dar es Salaam jana kabla ya kuanza kwa kikao cha siku mbili cha Kamati Kuu ya Chadema (CC), Mbowe alisema Rais Kikwete si mtu wa kupanga naye ‘dili,’ na kutolea mfano makubaliano kati ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na Rais kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Tulikutana na Rais Kikwete katika kikao cha TCD na kukubaliana kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ufanyike Februari mwakani ili tubadili sheria kwanza na kuboresha daftari la wapigakura.
“Cha ajabu kupitia kwa Waziri Mkuu, Serikali inasema uchaguzi utafanyika Desemba mwaka huu,” alisema Mbowe.
TCD inaundwa na vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni ambavyo ni CCM, CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi, UDP na TLP, huku vyama visivyo na uwakilishi bungeni vikiwakilishwa na chama cha UPDP kinachoongozwa na Fahm Dovutwa.
Kwa mujibu wa kanuni zilizotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu ambayo kisheria ndiyo yenye jukumu la kusimamia uchaguzi huo, fomu ya mgombea uenyekiti wa kitongoji ina sehemu 12 ambazo mgombea anatakiwa kujaza, ikiwamo nembo ya chama chake cha siasa na nembo ya halmashauri aliyopo.
Wakati huohuo, wanachama tisa wa Chadema Mkoa wa Njombe akiwamo Diwani wa Kata ya Njombe Mjini, Aggrey Mtambo wamekamatwa na polisi kwa mahojiano ya saa nne baada ya kuingia eneo la Kituo cha Polisi kwa ajili ya kufanya usafi kwa kile walichoeleza kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 15 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Tukio hilo lilitokea saa nne asubuhi jana na viongozi hao wa Chadema walishikiliwa hadi majira ya saa tisa alasiri walipowekewa dhamana.
Chadema walifika zilipo ofisi za polisi wilayani Njombe, kwa lengo la kufanya usafi katika kituo hicho, baada ya kufanya usafi katika Soko la Wakulima, Soko Kuu na Stendi Kuu ya Mkoa.
Mtambo aliliambia gazeti hili muda mfupi baada ya kuachiwa kwa dhamana kwamba, walikamatwa na kuwekwa ndani kwa kuwa walifanya usafi eneo la polisi bila kibali.
“Kwa mujibu wa polisi, wametukamata kwa kuwa tulienda kufanya usafi bila kibali na gari la taka tuliloenda nalo ni kama tulitaka kuteka kituo, , ” alisema Mtambo.