Meli ya MV Victoria ni Janga Linalosubiri Kutokea, Yapewa Jina la ‘Jeneza Linalotembea’.

Kwa muda wa wiki moja sasa, vyombo vya habari nchini vimekuwa vikiripoti hali mbaya kiusalama inayoikabili meli kongwe nchini, MV Victoria ambayo imekuwa ikisafirisha abiria na mizigo katika Ziwa Victoria kwa zaidi ya miaka 50 sasa. Tunaungana na vyombo hivyo vya habari kupaza sauti na kuihadharisha Serikali kuhusu janga la kitaifa linaloweza kutokea muda wowote kuanzia sasa, kutokana na meli hiyo kuzeeka kiasi cha kupata hitilafu mara kwa mara na kuhatarisha maisha ya abiria.

Hali hiyo inatokana na tukio la usiku wa kuamkia Jumamosi ya wiki iliyopita, ambapo abiria 381 waliokuwa katika meli hiyo ikiwa safarini kutoka Bukoba kwenda Mwanza walinusurika kifo. Habari zinasema meli hiyo ilipata hitilafu katika usukani na baadaye injini zake kuzimika zaidi ya mara mbili kabla ya kujikongoja hadi Bandari iliyo karibu ya Kemondo. Kwa muda mrefu sasa, zimekuwapo habari za matukio mengi ya kutisha ambapo meli hiyo imekuwa ikipata hitilafu ikiwa safarini kati ya Mwanza na Bukoba, kiasi cha kupewa jina la ‘jeneza linalotembea’.

Tunaambiwa abiria wanasafiri kwa hofu kubwa, huku roho zao zikiwa mikononi, kutokana na matatizo ya kiufundi yanayosababisha meli hiyo kuchelewa kufika bandari za Mwanza na Bukoba tofauti na ilivyokuwa zamani. Abiria wamekuwa wakiandamwa na matukio mengi yanayoleta hofu na kuashiria meli hiyo inaweza kuzama wakati wowote.

Tukio la mwaka 1996, ambapo MV Bukoba ilizama na kuua abiria zaidi ya 1,000 katika ziwa hilo halijasahaulika kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa, ambao hivi sasa wanahoji iko wapi meli mpya waliyoahidiwa na Rais Benjamin Mkapa baada ya kutokea ajali ile. Vilevile, wanahoji wapi ilipo meli mpya waliyoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, hasa wanapotilia maanani kwamba amebakiwa na mwaka mmoja tu wa kuwa madarakani.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Hivi kabisa watu na akili zao wa naamini wanasiasa wanapotoa ahadi hewa???? Tena kipindi cha campaign hahahaaaaa nicheke me nilie nina machozi???

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad