Hali za watoto pacha waliozaliwa wakiwa wameungana, Eliud na Elikana wenye mwaka mmoja na miezi sita, zinazidi kuimarika tangu walipofanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya Julai mwaka huu.
Watoto hao, ambao mwaka jana walifanyiwa upasuaji wa kuwatenganisha India, walilazwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya kufanyiwa matibabu ya marekebisho madogo ya kuziba njia za kutolea haja kubwa na kuwekewa njia ya kudumu.
Hata hivyo, kabla ya kufikishwa hospitalini hapo, Eliud alifanyiwa upasuaji wa aina hiyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dar es Salaam na alipopelekwa Mbeya alifanyiwa tena marekebisho.
Upasuaji huo ulifanywa na Daktari Bingwa wa Upasuaji, Kitengo cha watoto Muhimbili, Dk Zaituni Bokhary.
Wakizungumza nyumbani kwao katika Kijiji cha Kusumulu, Kyela juzi, wazazi wa watoto hao walisema afya za pacha hao zinaendelea kuimarika siku hadi siku, kwa kuwa vidonda vyao vimepona na wana furaha muda wote.
“Kwa kweli tunamshukuru Mungu, kama unavyowaona maendeleo yao ni mazuri, sasa Elikana ameanza kutembea kabisa na huyu mwenzake Eliud, bado ila ameanza kutambaa na hata uzito wanaongezeka.
“Elikana ameongezeka hadi kufikia kilo 13 kutoka kilo 10 alizokuwa nazo Agosti mwaka huu na Eliud amefikisha uzito wa kilo tisa kutoka kilo saba,” alisema mama yao mzazi, Grace.
Alisema kutokana na kuendelea vizuri kwa watoto wake, wanasubiri muda ufike wa kufanyiwa tena upasuaji mdogo wa njia ya mkojo.
Alisema waliambiwa na Dk Bokhary kwamba Mei mwakani watatakiwa kurudi India ili wakafanyiwe upasuaji tena.
“Wakati ule tukiwa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk Zaituni alituambia kwamba Desemba atarejea kutoka masomoni na Mei mwakani watatakiwa kwenda India kufanyiwa upasuaji wa njia ya mkojo na kuwekewa ya kudumu, hivyo tunamsikiliza yeye,” alisema.
Baba mzazi wa watoto hao, Erick Mwakyusa alisema wanaye wanamletea faraja kubwa kwani hata ile tabia ya kuchagua chakula walivyokuwa nayo awali, hawana tena na badala yake wanakula chakula chochote wanachopewa.
“Kutokana na uchumi wetu kutokuwa mzuri sana, hata chakula wanakula kile tunachokuwa tumepika siku hiyo na kwa bahati nzuri hata wao hawasumbui kama ilivyokuwa awali japo daktari wao alituhimiza zaidi kuwapatia maziwa na sisi tumekuwa tukifanya hivyo mara kwa mara,” alisema.
Aliishukuru Kampuni ya Mwananchi Communications Limited kwa kuwa karibu na familia yake kwa kipindi chote huku akibainisha kwamba imekuwa msaada mkubwa wa kufanikisha matibabu ya watoto wake.
“Bila ya ninyi waandishi wa Mwananchi, sijui hali yangu na watoto wangu ingekuwaje, msaada wenu ndiyo umenifanya niweze kukabiliana na hali halisi kwani ndiyo umenifanya nipate pikipiki ambayo kwa sasa ndiyo mkombozi wa familia yangu,” alisema.
Mungu Mkubwa Wale Watoto Pacha Waliotenganishwa India Sasa Waanza Kutembea
0
October 07, 2014
Tags