MWANASHERIA Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, jana alinusurika kupigwa na wajumbe wenzake wa Bunge Maalumu la Katiba baada ya mwanasheria huyo kupiga kura ya wazi ya “hapana,” kukataa rasimu ya Katiba inayopendekezwa na Bunge hilo.
Awali, Othman alikuwa amesusia Bunge hilo na kujiuzulu katika kamati ya uandishi iliyoandaa rasimu hiyo, akidai kwamba hoja 17 za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimepuuzwa katika katiba mpya.
Jana asubuhi, mwanasheria huyo aliingia ghafla ukumbini, muda mfupi baada ya Bunge kuanza huku baadhi wajumbe ambao hawakuwepo wakati wa kupiga kura, wakiwa wamemaliza kufanya hivyo, lakini wakati Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta, akimalizia matangazo ili kuahirisha Bunge. Ndipo alipotaarifiwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar alikuwa amefika, apewe nafasi ya kupiga kura.
Othman alisimama taratibu, kwa kusitasita mithili ya mtu aliyelazimishwa, akasema, “napiga kura ya wazi, na vifungu ambavyo sivikubali ni ibara ya 2, 9, 70, 71,72,73,74, 75, 128,129,158,159,160,161,243 hadi
251 na nyongeza ya kwanza, vingine vilivyosalia navikubali.”
Vifungu alivyokataa vinahusu mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (2), ukuu wa katiba (9), muundo wa muungano (70), utekelezaji wa shughuli za mamlaka ya nchi (71), mamlaka ya serikali ya jamhuri ya muungano (72) na mamlaka ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar yasiyo ya
muungano (73).
Uhusiano kati ya serikali ya jamhuri ya muungano na serikali ya Mapinduzi Zanzibar (74), wajibu wa viongozi wakuu kulinda muungano (75), madaraka ya kutunga sheria (128), utaratibu wa kubadilisha katiba (129), SMZ na mamlaka yake (158), Rais wa Zanzibar na mamlaka yake (159), Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na kazi zake.
Baraza la Wawakilishi la Zanzibar (161) na kuanzia ibara ya 243 hadi 25, inahusu Mfuko Mkuu wa Hazina na Fedha za Jamhuri ya Muungano wakati nyongeza ya kwanza ni kuhusu mambo 16 ya muungano.
Baada ya Othman kupiga kura hiyo, Bunge lilionekana kutaharuki hususani wajumbe kutoka Zanzibar, na muda mfupi baadaye alisimama Yahaya Kasimu Issa na kuomba aruhusiwe aseme kidogo.
“AG amepiga kura wakati kwenye mjadala hakuwepo… na si kwamba alikuwa anaumwa bali kwa kejeli yake ya kuonesha kwamba amesoma.
“Tulitegemea awepo hapa tangu mwanzo lakini yeye akatoroka…hivi mwanasheria kama huyu ana maslahi gani kwa Wazanzibari? Yaani Rais amemteua awe msaidizi wake wa kazi lakini yeye ametoroka…hivi unaweza kutuambia tuna maslahi gani na mtu kama huyu?” Alihoji huku akishangiliwa.
Wajumbe wenzake wa Zanzibar walianza kupiga makofi na kumzomea mwanasheria huyo wakimwita “kamanda aliyekimbia vita, msaliti, UKAWA, hafai aondoke,” na kejeli nyingine, lakini yeye alikuwa mtulivu tu kwenye kiti chake.
Baada ya kuona vurugu hizo, Sitta aliinuka na kutangaza kufunga mjadala huo huku akiwataka wajumbe waache kumwandama mwanasheria huyo kwa kuwa kikatiba na kisheria, anao uhuru wa kuamua anavyoona inafaa kwani mle ndani hajaingia kwa wadhifa wake bali amepiga kura kama mjumbe.
Kauli hiyo ya Sitta, haikufua dafu kwani baada ya Bunge kuahirishwa,Wazanzibari wengi waliendelea kumzomea huku wakiinuka kwenye viti na kuanza kumfuata wakitaka kumpiga.
Baadhi ya viongozi wakuu wa Zanzibar, wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Idd waliingilia kati na kisha askari wa Bunge walizingira eneo hilo na kumwondoa wakimpitisha mlango wa viongozi wakuu.
Maigizoo kwanilazima akubaliane nanyie.mumpige nyie ndiomnahaki sana sinae anauhuru wake.comedy
ReplyDelete