Shirika la Ndege la Fast Jet Lalamikiwa Kuwa ni Kimeo, Wateja Walalamika

Stori: Ojuku Abraham
SHIRIKA la Ndege la Fast Jet linalotoa huduma ya usafiri wa anga katika baadhi ya mikoa ya Tanzania na nje ya nchi, limelalamikiwa na wateja wake mbalimbali kutokana na jinsi linavyofanya kazi, Risasi Jumatano lina habari kamili.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, baadhi ya wateja hao wamesema kuwa, matangazo ya kila siku kuwa shirika hilo linatoa huduma ya usafiri wa anga kwa bei nafuu ni usanii, kwani tiketi zinazouzwa kwa bei hizo ndogo, daima huelezwa kuwa zimekwisha.

“Wanatangaza kuna tiketi za shilingi 32,000, ni uongo, mimi binafsi nimewahi kuulizia hizi tiketi mara kadhaa, lakini kila nikiomba ninaambiwa zimeisha na hata ndani ya ndege sijawahi kukutana na msafiri mwenye tiketi ya bei hizo,” alisema Samuel Kuntu, mkazi wa jijini Mwanza.

Aliongeza yeye amewahi kusafiri mara kadhaa na ndege za Fast Jet, lakini amegundua upungufu mkubwa wa shirika hilo, ikiwemo nauli kubwa tofauti na inavyotangazwa kwenye vyombo vya habari.
“Jana (Jumapili iliyopita) nilikuja na ndege hii na nimelipia shilingi laki nne kwa safari ya Dar, bei hii ni kubwa, nadhani ATCL ndilo shirika lenye bei rahisi, lakini si hawa,” alisema Kuntu ambaye alionekana kujua mengi kuhusu Fast Jet.
Alisema shirika hilo la ndege lina utaratibu unaomuumiza mteja hasa pale anapoahirisha safari au kuchelewa ndege, tofauti na mashirika mengine kama Precision Air na Air Tanzania.
“Inapotokea abiria amechelewa ndege (no-show), Fast Jet humtaka alipe tiketi nyingine na kulipa asilimia 100, wakati mashirika mengine humtoza faini abiria ambaye amechelewa ndege kwa asilimia 25 ya bei aliyonunulia tiketi kisha kumpangia siku nyingine ya safari.

“Wakati mwingine wanaahirisha safari au ndege kuchelewa lakini mteja hafidiwi kwa chochote, ila mteja akichelewa, harudishiwi hata shilingi wala kupangiwa siku nyingine, alisema mfanyabiashara huyo anayesafiri mara kwa mara kati ya Mwanza na Dar es Salaam.

Msafiri mwingine , Sunday Shomari ambaye alisafiri na ndege hiyo akitokea Arusha kwenda Dar es Salaam, alisema alisahau simu yake ya mkononi ya gharama kubwa pamoja na Ipad yake ndani ya ndege hiyo, lakini muda mchache baada ya kurejea hakupata vitu vyake.

“Nilikuwa na mke na watoto tunatoka Arusha, tulipofika Dar es Salaam tukashuka na kuvisahau vitu hivyo kwa bahati mbaya, tulipofika nje mke wangu akaniuliza simu yako ipo wapi? Nikakumbuka nimeisahau ndani ya ndege, nikarudi uwanjani na kuwaomba walinzi wanisaidie niende nikachukue simu yangu.
“Wakaniambia wao hawana mamlaka ya kuingia ndani ya ndege ile, badala yake wakanisaidia kuwaambia wafanyakazi wa ndege kuwa waniangalizie vitu vyangu pale nilipokaa, lakini jambo la ajabu eti wakadai hawakuviona, wakati mimi nilikuwa msafiri wa mwisho kushuka kwenye ndege, ina maana hakukuwa na mwingine baada ya mimi kushuka ambaye ningeweza kusema l ndiye aliyechukua vile vitu,” alisema Shomari ambaye ni mtangazaji wa zamani wa ITV na Radio One, kwa sasa anafanya kazi Sauti ya Amerika (Voa) jijini Washington, Marekani.

Abiria mwingine aliyekataa jina lake kutajwa gazetini, alisema mshangao mwingine kwenye ndege za shirika hilo ni kuuziwa vitu ambavyo katika mashirika mengine, wasafiri hupewa bure akitolea mfano soda, bia na viburudisho vingine.

Mwandishi wa habari hizi alifika katika ofisi za Fast Jet zilizopo Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutaka maelezo ya uongozi kuhusu tuhuma hizo, lakini walinzi walimzuia kuingia ndani na kutakiwa kuchukua anuani ya barua pepe ya msemaji wake, kwa maelezo kwamba ndiye angeweza kumsaidia kwa mambo ya kihabari.

Mwandishi aliandika madai yote na kuyatuma kwenye anuani hiyo akitaka kuonana na uongozi kwa ajili ya kujibu maswali kadhaa, lakini afisa uhusiano aliyejibu ujumbe huo, Lucy Mbogoro, baadaye alilitaka gazeti hili kuandika maswali hayo na kuyatuma, sambamba na nakala ya sura ya mbele ya gazeti.
Lakini hata baada ya kutuma maswali hayo kama ilivyotakiwa, Fasjet wameshindwa kutoa majibu na Lucy alipopigiwa simu na kuulizwa, alidai anayehusika na majibu hayo ametingwa na kazi.

Hata hivyo, gazeti hili bado linafuatilia kwa karibu ili kupata majibu ya maswali hayo.
GPL


Post a Comment

6 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Kweli kabisa wanakera sana! Wanathamini maslahi yao tu bila kuwafikiria na wateja.

    ReplyDelete
  2. ndiyo maana shirika lao la kwanza lilibuma nahisi na hili linaelekea hukohuko

    ReplyDelete
  3. Not true, wengine tumewahi kupata hizo tckt za bei rahisi. Kwenye kuchelewa Kweli hawarefund lakini waTz tuache sababu na tujifunze kuwa punctual

    ReplyDelete
  4. Sipingani nawe kdg coz hizo tiketi za bei rahisi zinapatikana mara chache tena ukiwahi kukata mwezi au miezi miwili hadi mitatu kabla ya safari. Pia Ukichelewa hawakujali na wala ikitokea wao wameahirisha safari hawakujali pia. Fikiria mwingine unaishi mbali sana na airport then unafika unaambiwa sorry leo ndege hakuna hadi kesho na mfukoni huna kitu unafanyaje hapo? Tuongee ukweli jamani na siyo kwamba nawaponda ila ukweli ndio huo.

    ReplyDelete
  5. kuna ishu mbili tu za fastjet ambazo naona si sawa.

    1. Uaminifu, kama sunday alivyopoteza vituvyake ilibidi vipatikane.
    2. wanapovizia dakika 40 za mwisho na kufunga geti. Ukichelea hata dakika mbili kwenye fastjet jua kwamba ticket yako imekwenda na maji. Huu ni unyang'anyi kabisa.

    mengine yote ni sawa. cheap airline zina low price unapobook in advance, na hiyo ndio trick. Kumbuka hiyo ni price bila kodi yoyote. hivyo 32000 hufika hadi 50,000 unapobook in advance.
    Poleni wote kwa fastjet

    ReplyDelete
  6. Wadau wote nimewakubali lakini tunaomba wabadilishe baadhi ya sheria zao maana zinaumiza na ni mwanzo wa kujichafulia jina, tunaomba waweke utaratibu wa mtu anapoachwa na ndege wamchaji pelnati kidogo lakini sio kununua ticket mpya kama wanavyofanya.

    emagine mtu kanunua ticket kwa 700000 afu kachelewa ndege hasaidiwi kwa lolote zaid ya kununua ticket mpya huo uwizi1!!!!!!!!!!! PILI tatizo lingine ni kwenye kubadilisha ticket unabadilishiwa kwa gharama kubwa sana kana kwamba unanunua ticket nyingine sio kama mashirika mengine ukitaka kubadilisha kama class zinafanana hauchajiwi kabisa na kama zikitofautiana unachajiwa hela kidogo tu kama 30000....nimetoa hii comment nikiwa kama agent ninaefanya nao kazi tunapata malalamiko kutoka kwa wateja wetu wanaona kama tunawaibia.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad