Ukawa Sasa Waja na Tuhuma Nzito Kuhusu kura za Bunge la Katiba

Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeibua shutuma dhidi ya uongozi wa Bunge Maalumu la Katiba kwamba unawarubuni kwa fedha baadhi ya wajumbe wa umoja huo ili kuipigia kura Katiba inayopendekezwa.

Kamati ya Ufundi ya Ukawa, ilisema jana kuwa wajumbe wanaorubuniwa wapige kura ya ‘ndiyo’ kwa ahadi ya kupewa zaidi ya Sh500 milioni ni wa CUF na wengine wanne wa Chadema wanaotoka Zanzibar.

Hata hivyo, Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Khamis Hamad alikanusha madai hayo, akisema hajasikia kitu kama hicho na ndiyo kwanza alikuwa anasikia hilo kutoka kwa mwandishi wa habari hizi... “Hakuna kitu kama hicho, hilo jambo ndiyo nalisikia kutoka kwako.”

Kutokana na madai hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ukawa, John Mnyika alisema kamati hiyo ilianza kikao cha siku mbili kuanzia jana kujadili hali hiyo na kutoa mapendekezo kwa uongozi wa juu wa umoja huo.

Licha ya Mnyika kukataa kutaja majina ya wajumbe waliorubuniwa, wajumbe wa Chadema wanaotokea Zanzibar ni Zeudi Abdallah ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Maryam Msabaha, Mwanamrisho Abama na Raya Ibrahim. “Tumewataka wajumbe wetu wote kukusanya ushahidi na kuuwasilisha kwa viongozi wa Ukawa,” alisema Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara.

Aliongeza, “Chadema ina wajumbe wanne, watatu ni wabunge wa kawaida na mmoja wa kuteuliwa na Rais (Kundi la 201). Tumepata taarifa kutoka kwa wajumbe hao kwamba wanapigiwa simu na uongozi wa Bunge ukiwataka wasaini karatasi za kupigia kura ili uongozi wa Bunge uchakachue kura.

“Tumeanza kikao kujadili suala hili ila tumeamua kwanza tuueleze umma kupitia vyombo vya habari juu ya ‘uharamia’ unaofanywa na Bunge la Katiba linaloongozwa na Sitta (Samuel) na Makamu wake Samia (Suluhu Hassan).”

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Mungu wabariki wasizikubali hizo hela

    ReplyDelete
  2. Mungu tuepushe na haya mafisadi, eeh Mungu bariki Tanzania

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad