Mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji (39), ametajwa kuwa ndiyo bilionea namba moja nchini kwa sasa, akifuatiwa na Rostam Aziz (49).
Kwa mujibu wa ripoti ya Jarida la Ventures Afrika lililotolewa jana, wafanyabiashara hao ndiyo Watanzania pekee waliongia kwenye orodha ya mabilionea 55 barani Afrika.
Dewji, ambaye pia ni mbunge wa Singida Mjini kwa tiketi ya CCM, ni mfanyabishara kijana aliyekamata nafasi ya 24 katika orodha hiyo akiwa na utajiri wa Dola 2 bilioni Marekani (Sh3 trilioni).
Nafasi hiyo inamfanya kijana huyo kutambulika kama tajiri namba moja nchini kwa sasa na siyo tena Rostam.
Katika orodha hiyo Dewji amemwacha Rostam kwa nafasi 16. Rostam anashika nafasi ya 40 akiwa na utajiri wa Dola 1.2 bilioni za Marekani.
Mwaka jana, Rostam alitajwa kuwa ndiye tajiri namba moja Tanzania. Hiyo ilikuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na jarida la Marekani la Forbes. Rostam alikamata nafasi hiyo na ya 27 katika Afrika akiwa na utajiri wa Dola 1 bilioni za Marekani (Sh1.6 trilioni).
Katika orodha hiyo, yumo pia Said Bakhresa ambaye aliwahi kutajwa siku za nyuma kuwa mmoja wa mabilionea wa Tanzania na Afrika.
Hata hivyo, ripoti ya jarida hilo ya mwaka 2011, ilimtaja Bakhresa kuwa ndiye aliyekuwa tajiri namba moja wa Tanzania. Bakhressa katika kipindi hicho alikadiriwa kuwa na utajiri wa Dola 620 milioni (Sh971 bilioni) akifuatiwa na Rostam, Mengi na mfanyabiashara mwingine maarufu, Ali Mufuruki.
Mengi alishikilia nafasi ya pili Tanzania na 34 Afrika akiwa na utajiri wa Dola 550 za Marekani (Sh861 bilioni).
Forbes ilionyesha kuwa Bakhresa alifungana na Mo katika nafasi ya tatu ya orodha ya matajiri wa Tanzania na ya 38 kwa Afrika. Wote walikuwa na utajiri wa Dola 500 milioni (Sh783 bilioni). Jarida hilo limemtaja pia tajiri kijana wa Nigeria mwenye umri sawa na Dewji, Igho Sanomi kuwa anashika nafasi ya 30 akimiliki Dola 1.3 bilioni.