Dr. Slaa anasa Mawasiliano ya siri kuhusu utafiti uliofanywa na TWAWEZA

Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza kuhusu maoni na matakwa ya wananchi juu ya uongozi wa kisiasa nchini, umeibua madai mapya ambayo yanauhusisha na jitihada za kukisaidia chama tawala CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa Dar es Salaam juzi, inaonyesha kuwa kama Uchaguzi Mkuu ungefanyika sasa, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa angeshinda urais kwa asilimia 13, akifuatiwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa asilimia 12, huku Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa akiibuka na asilimia kumi na moja.

Mbali na wanasiasa hao, wengine waliotajwa katika ripoti hiyo na asilimia zao kwenye mabano ni Profesa Ibrahim Lipumba (6%), Dk John Magufuli (3%), Freeman Mbowe (3%), Samuel Sitta (4%), Bernard Membe (5%) na Zitto Kabwe (1%).

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa iwapo vyama vyote vya upinzani vitaungana na kumchagua mgombea mmoja wa urais, Dk Slaa angeongoza kwa asilimia 41, akifuatiwa na Profesa Lipumba (14%), Mbowe (11%) na Zitto Kabwe (6%). Wengine ni Tundu Lissu, Maalim Seif Sharif Hamad, James Mbatia na Augustine Mrema ambao kila mmoja aliambulia asilimia moja.

Dk Slaa

Akizungumzia utafiti huo jana, Dk Slaa alisema chama chake kinautilia shaka kwani licha ya kuonyesha kwamba umefanywa na taasisi ya Twaweza, taarifa alizonazo zinaeleza kuwa matokeo yake yameandaliwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana.

Dk Slaa alisema Dk Bana anafahamika kuwa na uhusiano na CCM na kwamba pia anafanya kazi na taasisi nyingine ya utafiti ya Redet jambo linaloonyesha kuwa utafiti huo umeandaliwa kwa manufaa ya CCM.

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti jana, madai hayo yalikanushwa na Mkurugenzi wa Twaweza anayemaliza muda wake, Rakesh Rajani na Dk Bana.

Dk Slaa alisema kuwa amepata taarifa alizoziita za kutisha kuwa mmoja wa viongozi nchini (hakumtaja jina) alituma baruapepe kwenda kwa kiongozi mwingine akimwambia kuwa bosi wake atafurahi kwa kuwa kazi aliyowatuma wameimaliza.

“Taarifa hii imetushtua na tunaendelea kuifanyia kazi,” alisema Dk Slaa. Alisema alisoma ripoti ya Twaweza siku tano kabla ya uzinduzi na kwamba alibaini kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wananchi waliohojiwa walikuwa ni wazee.

“Tunataka kujua jambo hili lilifanyika kwa makusudi au lilikuwa na maana gani?”

Katibu Mkuu huyo aliikosoa ripoti hiyo kuwa iliwezaje kutabiri mambo kabla hayajatokea kwa kueleza kuwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ungeungana na kumsimamisha mgombea mmoja wa urais.

“Ukitazama taarifa imetolewa lini na maswali yaliulizwa lini utashangaa. Kwa nini unaweka mkokoteni mbele ya punda?” alihoji Dk Slaa. Hata hivyo Twaweza katika ripoti yake inaeleza bayana kwamba iliuliza swali kuhusu mgombea mmoja wa upinzani ikiwa vyama hivyo vitaungana.

“Wakati tunafanya utafiti huu vyama vinavyounda Ukawa vilikuwa havijasaini makubaliano ya kuwa na mgombea mmoja lakini kwa sababu tulishaona dalili na kusikia tetesi, basi tuliamua kuuliza swali hili. Kwa hiyo kwa kuwa sasa tayari vyama hivyo vimeshasaini makubaliano, utafiti mwingine unaweza kuwa na matokeo tofauti kabisa,” alisema Mwasilishaji wa Utafiti huo, Elvis Mushi juzi.

Rakesh atoa ufafanuzi

Akizungumzia tuhuma za kumtumia Dk Bana kufanya utafiti huo, Rakesh alisema siyo za ukweli kwa kuwa matokeo yanaonyesha kuwa walioshinda ni wananchi asilimia 33 ambao hawajaamua kumpigia kura mgombea wa chama chochote.

“Siwezi kusema kama Dk Bana anatumiwa na CCM, lakini ninachojua ni kuwa tulimwalika kushiriki kama mchangia mada kama watu wengine walivyofanya,” alisema.

Kuhusu kundi la wananchi ambao hawajaamua mtu wa kumpigia kura, Rakesh alisema ni vyema hata kama mtu angesema CCM haifai kutokana na matokeo hayo kwa kuwa wagombea wote wamepata chini ya asilimia 15.

Alisema watu wanaoisoma ripoti hiyo kwa kuangalia majina ya watu maarufu wanafanya makosa kwa sababu mwanafunzi hawezi kushangilia kwa kupata maksi ndogo.

“Hivi wewe ukipata mtihani mmoja asilimia 13 na mwingine 33, upi utakuwa umefaulu?” alimhoji mwandishi na kuongeza: “Asilimia 33 ndiyo unakuwa umefaulu.”

Alisema Twaweza imefanya tafiti za Sauti za Wananchi mara 24 na kwamba wamekuwa wakifanya kwa uadilifu wa hali ya juu. Alifafanua kuwa Watanzania wanafurahi pale matokeo ya utafiti yanapokuwa mazuri kwao, lakini hukasirika yanapokuwa kinyume.

Dk Bana ajitetea

Kadhalika, Dk Bana alikanusha tuhuma zilizotolewa na Dk Slaa dhidi yake akisema hajawahi kuwa na uhusiano na Twaweza huku akidai kuwa hata yeye mwenyewe anatamani CCM itoke madarakani miaka mitano tu, ili wananchi wapate uongozi tofauti.

“Kwa kweli ningekuwa na simu ya Dk Slaa ningempigia. Chadema na Ukawa wakijipanga wanaweza kuchukua nchi maana wana ushawishi mkubwa kwenye vyombo vya habari na makundi ya jamii.

“Kosa walilolifanya ni kumtimua Zitto Kabwe, ni kama vile Barcelona bila (Lionel) Messi. CCM sasa hivi imechokwa wananchi wanataka kuona uongozi tofauti,” alisema Dk Bana.

Alisema kitendo cha Chadema kumhusisha na CCM kitakwamisha mpango wake wa kujiunga na chama hicho ili agombee ubunge katika Jimbo la Bukoba Vijijini... “Ingawa familia yangu haipendi niingie kwenye siasa, bado naendelea kufikiri, lakini kwa mambo haya (Chadema) watanikubali kweli?” alihoji.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad