Geez Mabovu amefariki katika kipindi ambacho kwa asilimia kubwa alikuwa amepotea kwenye masikio ya wengi. Na mara nyingi sababu za kupotea kwenye masikio ya watu ni kutochezwa kwa nyimbo za msanii katika vituo vya redio.
Kwahiyo haimaanishi kuwa kupotea kwa msanii kwenye masikio ya watu kunatokana na ukimya wake mwenyewe bali ni kutopata nafasi ya nyimbo zake kuchezwa kwenye vituo vya redio zaidi hata kwenye TV.
Mara ya mwisho kukutana na Geez Mabovu na kuongea naye ilikuwa January 7 mwaka huu pale Msasani Club kwenye kilinge. Nilizungumza naye kwa kirefu na alikuwa mengi ya kueleza kutokana na kupotea kwake. Pamoja na wengi kutomsikia, Geez alikuwa akiendelea na harakati zake za kuachia ngoma.
Sauti yake nzito na uandishi wa akili ulikuwa bado uko vile vile. Siku za hivi karibuni afya yake ilikuwa imedhoofika kiasi pengine ni kutokana na kunywa sana pombe kali. Lakini hiyo haikuwa imeathiri uwezo wake wa pekee katika kuandika na kuchana.
Geez uliyemsikia kwenye ngoma zilizohit kama ‘Mtoto wa Kiume’ ‘Mimi’ na zingine ndiye yule yule aliyesikika kwenye wimbo wa hivi karibuni ‘U Can’t Stop Me Now’ aliomshirikisha Joh Makini na Nisher.
Huu ni miongoni mwa nyimbo za hip hop zilizotoka miaka miwili iliyopita na bora kabisa. Bahati mbaya wimbo huu haukupata nafasi na mashabiki wengi wa hip hop hawakupewa haki ya kuusikiliza. Pengine ulikuwa na nafasi kubwa ya kumrejesha tena kwenye chart. Iwapo wimbo mkali kama huo ulinyimwa nafasi, msanii arekodi wimbo wa aina gani ili apewe fursa? Hatuoni kama kuna tatizo sehemu? Tatizo ambalo linatakiwa kurekebishwa.
Redio hazikuutendea haki wimbo huo. Redio hazikumtendea haki Geez Mabovu. Redio zina deni kubwa kwa Geez Mabovu. Bahati mbaya deni hilo haliwezi kulipwa sasa. “Tulipofanya hii ngoma kwa Majani nikamwambia ‘Geez hii ngoma kali’ lakini mimi ndiye niliyekuwa namcheck sababu nilikuwa naiona ile ngoma,” amesema Joh Makini.
“Nilikuwa nahisi kuna matatizo yanamsumbua au labda ni life au stress whatever. Nilikuwa nikiuangalia huo muziki niliofanya na yeye na nikiulinganisha na muziki wa hip hop uliopo kwenye mainstream, nilikuwa naona muziki mkubwa sana ndio maana nilikuwa namuambia niachie huu muziki uwe wangu ili niupush wewe uwe kama umeshirikishwa.”
Haisadii tena kucheza nyimbo zake sasa hivi labda kama lengo ni kumuenzi, lakini si kwa kumsaidia yeye kuishi. Geez hatuko naye tena. Geez hahitaji tena show.
Redio hazikitakiwi kukumbuka kucheza nyimbo za wasanii wenye vipaji kama hawa wakifariki, haiwasaidii, inawaletea huzuni tu ndugu na mashabiki wake.
Sikumbuki ni lini katika miaka mitano iliyopita Geez Mabovu alitajwa kutumbuiza kwenye show yoyote kubwa. Mtu kama huyu ambaye anatagemea muziki anaishi vipi? Roma aliandika jambo la msingi na lenye ukweli kuwa hakuna watu wenye stress kama wasanii.
Kuna vipaji vingi vinapuuzwa sasa. Tunasubiri vipotee kabisa ndio tuanze kucheza nyimbo zao? “Wasanii kama Geez Mabovu tunao wengi sana hapa Tanzania lakini hatujifunzi kwa mifano,” anasema Roma.
“Kuna vipaji havipaswi kupuuziwa hata kidogo jamani vipeni support, hundred please. Hatatokea msanii kama Afande Sele, mi nakwambia hadi leo ni mkali sana huyu mtu. Hakuna rapper kama Jos Mtambo asikwambie mtu. Yule Enika yule ni anaimba jamani acha tu. Hawa vijana wa Tamaduni Music ni new faces zinazokuja vizuri sana wapewe support Joslin, MB Dog, hawa watu ni Almasi jamani. Tuna wasanii wakali kibao mi nakwambia Dojo na Kaya ni ny**o. Wataimba wote ila mtu kama Rama Dee ni hadithi nyingine ujue,” anasisitiza.
“Wito wangu tafadhali tuwasapoti na tuzidi kuwasapoti vijana wetu wenye vipaji,” Roma anatoa ushauri. “Najua wapo wenye matatizo lakini tusiikate tamaa tuzidi kuwaonyesha njia bora ya mafanikio.”
Nilizungumza na Joh Makini ambaye ameshawahi kufanya ngoma zaidi ya tatu na Geez Mabovu na wana historia ndefu naye. Joh anaamini kuwa hakitatokea kizazi cha muziki wa hip hop bora kama chao na hivyo kukipuuza ni kosa kubwa. “Hofu yangu ni kwamba industry ya hiphop itachukua muda sana kupata generation kama hii. Na pengine inaweza isitokee tena,” anasema Joh.
“Hicho kipaji cha Geez Mabovu, Ngwair, Langa, Joh Makini, Nako 2 Nako, Fid Q, Mapacha, sidhani katika miaka miwili ijayo tutakuwa na kizazi kama hicho. Tukiwa nacho pia tutakuwa tumebarikiwa,” anasisitiza rapper huyo ambaye yeye na wenzake Weusi waliamua kuahirisha show yao ya Mbeya wiki hii kwa heshima ya Geez.
Ngwair, Langa na Geez Mabovu wamefariki katika kipindi ambacho vyombo vya habari vilikuwa vimewapa mgongo. Kosa hili litaendelea kutokea kama tutashindwa kuvienzi vipaji vilivyopo sasa.
Badala ya kuanza kulaumiana katika kipindi ambacho maji yameshamwagika na hatuwezi tena kuyazoa, tujifunze kutokana na makosa na tuvipe nafasi vipaji vinavyostahili kupewa.
Credits:BONGO5.com