Hakika Wasomi Ndio Wanao Itafuna Hii Nchi

Makala: Sifael Paul
Hatuwezi kunyamaza! Kuhusu uchotwaji wa fedha nyingi za umma, za wavuja jasho Watanzania kiasi cha Sh. bilioni 306 zilizopotea katika Akaunti ya Tegeta Escrow kwenye Benki Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kununulia umeme wa Kampuni ya IPTL, pasi na shaka utakubaliana nami kuwa wasomi ndiyo wanaoitafuna nchi hii.

Hii ni kashfa kubwa hasa inapoonekana wajanja wachache ambao ni wezi wanaojulikana kwa majina ndiyo wanaohusika. Tukubaliane kuwa si kweli Tanzania haina wasomi, wataalam na wazoefu katika nyanja mbalimbali kiasi cha kushindwa kung’amua wizi huo uliopitia kwenye mikono ya wasomi waliobobea serikalini. Nitawagusa watajwa wachache.

Kuanzia kwenye Wizara ya Nishati na Madini, waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo ni msomi wa ngazi ya uprofesa aliyebobea katika masuala ya ‘jiolojia’ hivyo si kweli kwamba hakujua kikamilifu kazi yake katika masuala ya nishati ya umeme. Pia naibu wake, Stephen Masele naye ni msomi.

Wakati Eliakim Maswi anachukua nafasi ya ukatibu mkuu wa wizara hiyo baada ya David Jairo kukumbwa na kashfa, tuliamini kwamba mambo yatakuwa shwari kwa kuwa alionekana msomi mzuri. 
Hata hivyo, fedha ni shetani na la kuvunda halina ubani kwani ndiye anayetajwa kuratibu kila kitu kwenye sakata la wizi huo. Hapa nimegusa watu watatu tu wizarani hapo.

Huwezi kuamini wizara hiyo imejaa wasomi wa ngazi za udaktari (PHD), mainjia na wataalam lukuki. Inashangaza kuona tukiibiwa na wenyewe wapo maofisini wanapigwa kiyoyozi na kufurahia maisha na familia zao huku Watanzania wakitaabika.

Kuhusu Tanesco ndiyo usiseme, mkurugenzi wake, Mhandisi Felchesmi Mramba na bodi ya Tanesco imejaa wasomi. Nani kawaloga hata washindwe kuona tatizo katika mkataba wa IPTL hadi kuwe na wizi wa fedha za kutosha kujenga hospitali za hadhi ya Muhimbili zaidi ya kumi?

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Feredrick Werema ni msomi wa sheria kwa ngazi ya juu kabisa.Werema amepitia vyuo vikuu vikubwa duniani vikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha American Graduate School (Marekani).

Pia amepitia vyuo vingine huko Italia, Uingereza na Bolivia. Huko kote, Werema alibobea kwenye masomo ya mikataba ya ubinafsishaji wa makampuni ya umeme hivyo hakuwa mgeni kwenye sakata hili la IPTL na Tegeta Escrow kiasi cha kupoteza Sh. bilioni 306 kirahisi kiasi hicho. Labda kama alifumbwa macho asione.

Kwa upande wa Benki Kuu ya Tanzania, gavana wake, Profesa Benno Ndulu ni msomi mkubwa kwa ngazi ya uprofesa wa masuala ya uchumi akipitia na kufundisha vyuo vikuu kikiwemo North-Western huko Evanston, Illinois, Marekani. Pia amefanya kazi kwenye Benki ya Dunia hivyo anajua vizuri majukumu yake. Mbali na kichwa chake, pale Benki Kuu ya Tanzania anafanya kazi na wasomi wa kila namna kwenye nyanja ya uchumi.

Swali ni je, ilikuwaje fedha ikayeyuka kwenye akaunti hiyo ndani ya Benki Kuu? Ina maana wote walipigwa ganzi wasing’amue mchezo au nao walishiriki?

Huku akipachikwa jina la Mtoto wa Mkulima, akikalia kiti kilichoachwa na Edward Lowassa aliyejiuzulu Februari 7, 2008, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, anayeaminika kwa uadilifu amejikuta akiingia kwenye kashfa hii kwa kuwa tu ni mtendani mkuu wa serikali.

Kinachotokea kwa Pinda ni kuwaamini hao tunaowaita wasomi bila kuthibitisha na kujikuta akitoa kauli ambazo Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) imethibitisha kwamba fedha zilizopotea ni za umma na siyo za IPTL kama yeye alivyonukuliwa.

Ukiufuatilia mjadala huu utagundua kuwa hata watuhumiwa wa uchotaji wa fedha hizo si watu mambumbumbu bali ni wasomi, tena wa ngazi za juu wanaoitafuna nchi hii kama wanavyotaka.
Kati ya wanaotajwa wapo wasomi kama Profesa Anne Tibaijuka, mwanasheria Andrew Chenge na wengine wengi.

Nihitimishe kwa kuwahakikishia kuwa wasomi wengi nchi hii si wazalendo, waadilifu, waaminifu, wawajibikaji. Ni wala rushwa, wameoza na wamepumbazwa. Wanajali zaidi matumbo yao. Hawatufai na kwa sasa ni aibu kusimama mbele za watu na kujiita msomi.

Niamini mimi, wapo watu wasio na uprofesa wala udaktari lakini ni wazalendo wa taifa hili. Hao ndiyo tuwape nafasi ya kusimamia kwa dhati rasilimali zetu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad