IKIWA ni siku chache tu baada ya kutolewa kwa taarifa za kukabidhiwa kwa ripoti ya ukaguzi wa akaunti ya ESCROW, uliofanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), kwa spika na kamati ya mahesabu ya serikali PAC, mengi yameibuka.
Hali hiyo inatokana na kuwepo kwa mgawanyiko wa wabunge kuhusu na jambo hilo huku kila upande ukiwa na mtazamo wake tofauti juu ya jambo hilo, ambalo wabunge wengi wanaamini linapikwa na halizungumzwi ukweli.
Taarifa kutoka Dodoma zinasema kwamba wabunge wengi wameshitushwa na kuvuja kwa taarifa kuwa kamati ya PAC imelivalia njuga suala hilo, baada ya kushindwana kuafikiana mgao wa malipo kutoka kwa wamiliki wa kampuni ya IPTL/PAP ili kulizuia kulimaliza katika Kamati lisifike bungeni mapema mwaka huu.
Taarifa hizo zinasema kamati ya PAC iliwatumia mwanasheria aliyefahamika kwa jina la Albert Msando ambaye ni msaidizi wa kisheria wa Zitto Kabwe na Beatus Malima kujadili juu ya malipo watakayolipwa PAC ili kuidhibiti ripoti hiyo na namna ambavyo PAC ingetoa hukumu ya awali.
Vithibitisho ambavyo baadhi ya waandishi wameonyeshwa na baadhi ya wabunge hao, vinaonyesha mijadala iliyokuwa ikiendelea bungeni kuwa mingi ni ya kupikwa na ya kimkakati inayotokana na hasira za kutokupatiwa malipo waliyoomba PAP na hivyo kulitaka bunge lipigie mhuri kitu ambacho ni mgogoro unaotawali na maslahi binafsi.
Haijafahamika mara moja kwamba ni kiasi gani kimeombwa na kamati ya PAC kwa PAP ili walifunge jambo hilo, mlakini baadhi ya wabunge hao wamesema wapo tayari kuweka wazi kila kitu ili kila mtu avune alichopanda.
‘’Ni kweli kila mtu atavuna alichopanda, kama wanataka kutugeuza wabunge wote ni ‘Rubber stamp’ tuhalalishe hukumu inayotokana na hasira zao za kunyimwa mgao, basi wamegonga mwamba’’.
Alisema mmoja wa wabunge hao anayetokea chama kimoja cha upinzani akijibu kauli ya Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe aliyenukuliwa na gazeti moja hivi karibuni.
Hivi karibuni Filikunjombe, alisema katika gazeti hilo, kwamba kila mtu atavuna alichopanda katika sakata hilo, baada ya kupokea ripoti ya CAG kutoka kwa Naibu Spika, Job Ndugai.
Akizungumza kwa kujiamini, mbunge mwingine ambaye pia ameomba ahifadhiwe jina lake kwa sasa anasema ’’Hata Kamati yenyewe ya PAC imegawanyika vipande vipande, wakubwa wao wamevuta mzigo wa kutosha na wenzao wanawaburuza, halafu kazi nzima ya kamati inapelekeshwa kutoa sifa kwa watu wawili tu ambao ni Zitto na Filikunjombe, huu ni upuuzi’’.
Mbunge huyo alisema sisi sote ni wanasiasa, unafikiri nani atakuwa tayari kufanya kazi, halafu sifa ziwaendee watu wawili tu kwamba wao ndio wanaakili sana na wana uchungu sana na nchi.
‘’Hebu jiulize kamati ina wajumbe zaidi ya 20 lakini kila kitu zitto na deo wanajiweka kimbelembele, sasa na safari hii wanapoumbuliwa kwa madili yao ya rushwa wakae kimbelembele hivyo hivyo’’. Alisema mbunge huyo.
Hata hivyo, taarifa kutoka kwenye ripoti iliyovuja ya CAG haionyeshi kwamba kuna tatizo kwenye ukaguzi walioufanya wa akaunti ya ESCROW, badala yake umeibua madai mapya ambayo sio msingi wa uchunguzi walioagizwa kufanya.
Itakakumbukwa kwamba akaunti ya ESCROW ilifunguliwa rasmi Julai, 5 2006, wakati ripoti ya CAG inaonyesha mapungufu ya kuanzia Januar 2002 mpaka Desemba 2006 huku ripoti yenyewe ilipaswa kujikita kati ya 2006 mpaka 2013 ilipofungwa.
‘’Hatupaswi kuwaadhibu watu kwa sababu tu tunawachukia, au kwa sababu tunachuki na tofauti nao binafsi ama za kisiasa, sisi kama bunge ni lazima tufanye kazi zetu kwa kudhibiti hisia zetu, wanachokifanya kina Zitto, David Kafulila na Deo, ni chuki binafsi na si uzalendo kama wanavyotaka iwe, kama ni wazalendo wasingefanya kama haya wanayofanya’’. alisema mbunge huyo.
Alisema mbunge huyo, wabunge hao baada ya kuona ripoti ya CAG haiwatii hatiani serikali na wanaowachukia wao, wanalazimisha kusema kuwa kuna hasara ya bilioni 321. Waache kuwafanya wabunge watoto wadogo kwa kuwa kila kitu tunakijua.
Wakati hayo yakiendelea, jana asubuhi Mbunge wa Mtera-CCM, Livingstone Lusinde aliiomba mwongozo kwa Naibu Spika, Job Ndugai kuhusiana na kubana kwa ratiba katika suala la akaunti ya ESCROW huku jambo hilo likiwa na hamasa kubwa kwa watanzania.
“Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Kamati ya Uongozi ya Bunge iongeze siku au muda katika kujadili suala hili, kwa kuwa ni jambo kubwa linalohitaji kujadiliwa zaidi, tuna mengi tunayoyajua, makando kando ya wanaotuhumiwa na wanaotuhumu pia, kwa kuwa waswahili wana msemo mmoja ukimuona anayelia sana ujue ndio mchawi mwenyewe,’’alisema.
Alisema wabunge wanaolia sana kuhusiana na jambo hilo, wenyewe wana makando makando katika suala hilo kutokana na kuhusika kwa namna moja au nyingine katika sakata hilo, ambalo anaamini kujadiliwa kwa muda mrefu zaidi ndio jambo litakaloweka haki kwa kila mtu.
Hivyo, aliiomba Bunge iongeze siku zaidi kujaidli suala hilo, ambapo Naibu Spika Ndugai alisema atawasiliana na Kamati ya Uongozi ya bunge kuhusiana na mwongozo huo wa Lusinde ili ufanyiwe kazi kwa kuwa jambo hilo lina umuhimu mkubwa kwa taifa.