Interpol Yawasaka Wachina 30 kwa Ujangili wa Tembo

Siku tano baada ya Serikali kukanusha vikali ripoti ya Shirika la Kimataifa la Mazingira (EIA) iliyoihusisha China na utoroshaji wa meno ya tembo nchini wakati wa ziara ya Rais wa nchi hiyo, Xi Jinping mwaka jana, Shirika la Polisi la Kimataifa (Intepol), Tawi la Tanzania limesema linawatafuta raia zaidi ya 30 wa China ambao wanatuhumiwa kusafirisha meno ya tembo na kufanya uharamia wa kimazingira katika hifadhi za Taifa nchini.

Kauli ya Interpol inakuja huku kukiwa na mkanganyiko kuhusu kashfa hiyo iliyosambaa wiki iliyopita kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa ambayo hata hivyo, Serikali imekanusha kupitia Ikulu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Maliasili na Utalii huku ubalozi wa China nchini nao ukitoa tamko la kukanusha taarifa hizo.

Kamishna wa Interpol Tawi la Tanzania, Gustav Babile alisema jana kuwa raia hao wa China wanatafutwa popote walipo duniani na hivyo watakapopatikana watakamatwa.

“Tunawatafuta popote duniani kwa usafirishaji wa meno ya tembo na uharamia wa mazingira, wakipatikana watachukuliwa hatua,” alisema Kamishna Babile.

Alisema majina na idadi kamili ya Wachina wanaotafutwa ipo na endapo kuna umuhimu wa kutajwa, yatatangazwa.

Mpaka sasa, mtandao wa Interpol umeweka majina ya raia wawili wa China, Mingzhi Zhang na Deng Jiyun ambao wanasakwa kwa tuhuma za kusafirisha meno ya tembo.

Wanadiplomasia kutokaguliwa

Wakati ripoti hiyo ilidai meno hayo yalisafirishwa kwa ndege ya Rais wa China kupitia maofisa wa kidiplomasia wa nchi hiyo ambao hawakaguliwi, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema maofisa wataendelea kutokaguliwa kwa kuwa Serikali haiwezi kubadili sheria za kimataifa za maofisa hao kupata kinga ya kutokaguliwa wanapokuwa kwenye msafara wa Rais.

“Kwa ninavyojua, ukaguzi wa mizigo kwa misafara ya kidiplomasia unazingatia na kutawaliwa na sheria za kimataifa kwa hiyo Tanzania haiwezi kubadili tu kama Taifa,” alisema Balozi Sefue.

Hata hivyo, alisema ni vyema kama Wizara ya Mambo ya Nje ingezungumzia suala hilo la sheria za kutokaguliwa kwa mizigo ya maofisa wa msafara wa Rais.

“Ni sheria za kimataifa kwa hiyo ipo, mizigo ambayo inakidhi vigezo vya kimataifa vya kutofanyiwa ukaguzi na ipo ambayo haina vigezo hivyo,” alisema Sefue.

Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Katibu Mkuu wake, Michael Haule hawakupatikana jana kuzungumzia suala hilo lakini ofisa mmoja wa wizara hiyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini alisema: “Kwa kawaida mizigo ya wanadiplomasia hao hukaguliwa ila wao wenyewe ndiyo hawakaguliwi, hilo ndilo jambo msilolielewa, ingekuwa wamebeba kitu kingeonekana tu.”

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad