KAMPUNI ya Pan Africa Power Resources (PAP) imesema haina mahusiano ya kiumiliki na familia ya Rais Jakaya Kikwete, kama umma unavyoaminishwa kwa kuwekewa taarifa sizizo za kweli kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
Taarifa ya kupinga tuhuma hizo ilitolewa jana na Katibu na Mshauri Mkuu wa Sheria wa Kampuni ya IPTL inayomilikiwa na PAP, Joseph Makandege, alipozungumza na waandishi wa habari.
Hivi karibuni mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, aitwaye Miraji alisikitishwa na tuhuma hizo zinazotolewa dhidi yake kuhusishwa na umiliki wa kampuni ya PAP kwamba yeye na dada yake, Salama wanamiliki asilimia 50 za PAP kupitia Simba Trust, wakati si kweli.
Akizungumzia jambo hilo, Makandege alisema PAP inamilikiwa kwa asilimia 50 na Harbidher Sing Seth na Simba Trust, ambayo nayo inamiliki asilimia 50.
Kwa mujibu wa Makandege alisema majina ya wamiliki wa Simba Trust ni Settler Clive Anthony Cooke, Pamela Sethi na Hardeep Kaur Chaggar.
Alisema hakuna sehemu yoyote inayoonesha kuwa kuna majina yatokanayo na familia ya Rais Kikwete, wakiwemo watoto wake, ambao ni Salama na Miraji Kikwete, hivyo huo ni mwendelezo wa upotoshaji wa uongo unaofanywa na wanasiasa na baadhi ya watu juu ya IPTL.
“Taarifa zinazosambazwa katika mitandao zina lengo la kuichafua familia ya Rais Kikwete na IPTL na ndio maana tumeona tufafanue ukweli halisi wa jambo hili ili umma uelewe,”alisema.
Makandege alisema PAP/IPTL haipendi kuzungumza na vyombo vya habari kuhusiana na sakata la ESCROW linaloendelea bungeni kwa kuwa wanasubiri ripoti ya serikali.
“Tunasubiri ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Taifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),”alisema.
Hivyo, Makandege aliwataka Watanzania kuwa makini na taarifa zinazosambazwa katika mitandao kwa kuwa hazielezi ukweli wa jambo hilo