‘Mchezaji Mkude wa Simba Akitua Yanga tu Kazi imekwisha’

KOCHA wa Simba, Patrick Phiri amefichua siri moja kwamba kiungo mkabaji wake, Jonas Mkude, hana muda mrefu atasaini mkataba wa miaka miwili Msimbazi lakini endapo akishawishika na kukimbilia Yanga au Azam kazi yake itakuwa imekwisha kisoka kwani atakuwa amejimaliza.

Mkude ambaye amebakiza mkataba wa miezi sita na Simba amewaambia Yanga wanaomnyemelea wampe Sh80 milioni ahame Simba ingawa viongozi wa Mnyama wameanza mazungumzo naye na wameshamkabidhi gari jipya ili kumshawishi atulie.

 Akizungumza na Mwanaspoti Phiri ambaye ni raia wa Zambia, alisema hakuna shaka kwamba kwa sasa nchini hakuna kiungo aliye katika kiwango bora cha kuweza kukaba na kuchezesha timu kama alivyo Mkude lakini anatakiwa kuwa makini na uamuzi wake.

“Nafahamu soka ni kazi yake hilo halina ubishi, kwa uwezo wake sasa ni wakati wa kupata mafanikio makubwa kupitia kipaji chake, nafikiri hatakiwi kufanya kosa kuondoka Simba,  atulie hapa ajijenge kiakili kuhimili soka la ushindani,”alisema Phiri.

“Bado anahitaji kucheza Simba labda afikirie hivyo baada ya miaka miwili mbele atakuwa na akili ya kuweza kuhimili presha kubwa kama hiyo akihama sasa sawa lakini kuna uwezekano mkubwa wa kumaliza kipaji chake.”

Phiri alisema mara baada ya kusikia taarifa za kiungo huyo kutaka kuondoka alimwita na kuzungumza naye juu ya uwezekano wa kuendelea kubaki Simba na juu ya maisha halisi ya klabu hiyo.

“Akiondoka Mkude hali ya kikosi chetu itakuwa mbaya zaidi, kwa sasa ni kama lulu ndani ya kikosi, ni mchezaji wa kiwango cha juu ambaye kila klabu ingependa kuwa na huduma yake,” aliongeza.

“Baada ya kupata habari kuwa anamaliza mkataba wake nilimwita na kuongea naye, nilimwuliza juu ya maisha ya Simba kwa kipindi alichokuwa pale, nilimwuliza pia juu ya changamoto na kama anayafurahia maisha pamoja na sisi,” alisema Phiri na kuongeza

“Ameniambia hana shida na maisha ya Simba, ana furaha ya kuendelea kuwa pamoja na sisi hivyo nimeuomba uongozi ujitahidi kumalizana naye mapema, najua viongozi wangu ni watendaji hivyo mambo yatakwenda sawa.”

Wakati huohuo Phiri alisema kikosi chake kinaendelea vizuri na maandalizi ya mchezo wao ujao dhidi ya Ruvu Shooting ambapo ameweka nguvu kubwa katika kuhakikisha washambuliaji wake wanafunga mabao mengi pamoja na kuimarisha ulinzi.

“Wachezaji wapo kwenye hali nzuri, kila mmoja anajitahidi kutimiza majukumu yake, wiki hii nimeweka nguvu kubwa kwenye mbinu za ushindi, tutakata kushinda mechi ijayo,” alisema Phiri.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad