Utangulizi
Taarifa hii inatolewa kwa umma kutokana na ripoti mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari mitandao ya kijamii na taarifa iliyotolewa kwenye mjadala katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
1. Ufunguzi wa akaunti ya VIP engineering and Marketing (VIP)
Kampuni ya VIP engineering and Marketing ni kampuni ambayo imesajiliwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania. Kampuni hii ilifungua akaunti katika benki ya biashara ya Mkombozi na hivyo kuwa moja kati ya wateja wa benki. Benki ilijiridhisha na ilizingatia taratibu zote za ufunguzi wa akaunti husika kwa kuzingatia sheria za nchi na kanuni zinazozitaka benki kupata nyaraka muhimu kutoka kwa mteja wakati wa ufunguzi wa akaunti hiyo.
Nyaraka hizo ni pamoja na kuwepo kwa cheti cha usajili wa kampuni, kanuni za kampuni, idhinisho la kampuni kumruhusu moja kati ya wanahisa wake kuendesha akaunti pamoja na picha na hati ya kusafiria ya mhusika wa kuendesha akaunti hiyo.
2.0 Mauzo ya hisa za VIP
Kampuni ya VIP ilileta mkataba kwenye benki ya Mkombozi wa mauziano ya hisa za asilimia 30 baina ya VIP na kampuni ya Pan Africa Power Solutions (PAP) ambazo inamiliki katika kampuni ya IPTL. Mkataba huo ulisainiwa tarehe 19 Ogasti, 2013. Bei ya asilimia 30 ya hisa hizo ilikuwa ni dola za Marekani milioni 75. Katika kifungu namba 2.4 cha mkataba wao kinaelekeza fedha za mauzo ya hisa zilipwe kwenye akaunti ya VIP iliyopo benki ya Mkombozi. Mkataba huo wa mauziano ya hisa baina ya kampuni hizi mbili ulitambuliwa na hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania iliyotolewa na Jaji J.H.K Utamwa tarehe 5 Septemba, 2013.
3. Mchakato wa kulipa kodi ya serikali
Benki ilitambua kwamba katika mauziano hayo ya hisa ni lazima kodi ya Serikali ilipwe na hivyo iliizishauri pande zote mbili kupeleka mkataba husika katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kufanyiwa makadirio ya kodi husika. Tarehe 20 Januari, 2014 TRA iliiandikia barua kampuni ya VIP na nakala ya barua hiyo kuletwa kwenye benki ya Mkombozi. Katika barua hiyo TRA iliitaarifu kampuni ya VIP kuwa makadirio ya kodi yatokanayo na mauzo ya hisa ni shilingi 38,186,584,322.00 ikiwa ni kodi ya mauzo ya hisa ya asilimia 30 za mauzo ya hisa kutoka VIP kwenda kwa PAP.(Capital gains and stamp duty).
TRA pia iliiagiza benki ya Mkombozi kuhakikisha kuwa inalipa kodi hiyo kwa niaba ya VIP mara tu fedha zitakapoingia kwenye akaunti yake.
Malipo ya kodi ya shilingi 38,186,584,322.00 yalilipwa TRA kwenye akaunti 11120100 iliyopo katika Benki Kuu ya Tanzania na TRA ilikiri kupokea kodi hiyo kwa barua yake yenye kumbukumbu namba 3-4/100/100/223/4 ya tarehe 24 Januari, 2014.
4. Ufafanuzi wa mambo mbalimbali
4.1 Benki ya mkombozi kuhusika katika kusafisha fedha chafu
Fedha zote zilizoingizwa kwenye akaunti ya VIP iliyopo kwenye benki ya Mkombozi zilitokana na mauziano ya hisa kati ya VIP na PAP kwa mkataba uliotambuliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania. Chanzo cha malipo hayo ni kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya PAP iliyopo katika benki ya Stanbic na kuingizwa kwenye akaunti ya VIP iliyopo katika benki ya Mkombozi.
Fedha hizo zilihamishwa katika mafungu mawili. Fungu la kwanza ilikuwa ni shilingi 73,573,500,000.00 zilihamishwa kwa njia ya TISS kwa kumbukumbu namba 000000050720 ya tarehe 23 Januari, 2014 na fungu la pili ni dola za Kimarekani 22,000,000.00 zilihamishwa kwa TISS kwa kumbukumbu namba 000000050812 ya tarehe 23 Januari, 2014. Malipo mengine ya asilimia kumi ya mauzo ya hisa yalilipwa kwenye akaunti ya Mkombozi iliyopo Benki Kuu ya Tanzania. Kutokana na mchakato huo benki ya Mkombozi ilijiridhisha kuwa fedha hizo ni malipo halali na siyo fedha chafu.
Benki ya Mkombozi haijihusishi na utakasishaji wa fedha chafu na haramu katika uchumi wa Tanzania.
4.2 Malipo yatokanayo na akaunti ya VIP
Malipo toka kwenye akaunti ya mteja hufanywa kutokana na maelekezo ya mteja. Benki ikishajiridhisha kuwa fedha ya mteja ni halali na ipo kwa mujibu wa sheria na hamna zuio lolote toka katika mahakama hapa nchini hutekeleza malipo kwenye akaunti ya mteja kutokana na maelekezo yake.
Benki ilijiridhisha kuwa malipo yote yaliyofanywa kutoka kwenye akaunti ya VIP ni halali kwa kuwa chanzo cha pesa hizo ilikuwa ni halali kutokana na mauzo ya hisa na ulipwaji wa kodi ya Serikali kama ilinyoelezwa hapo juu. Kutokana na sababu hiyo benki haikuwa na shaka juu ya malipo hayo.
4.3 Malipo taslimu kwa wateja na kubeba fedha kwenye viroba, mifuko ya rambo na magunia
Benki inatoa tamko kuwa malipo yote yaliyofanywa katika akaunti ya VIP yalilipwa kupitia akaunti za walipwaji. Hakuna fedha zilizolipwa taslimu kwa wateja na kubebwa kwenye viroba au magunia kama ilivyoripotiwa Bungeni. Pesa iliyotoka kwenye akaunti ya VIP tarehe 6 Februari, 2014 kiasi cha shilingi 3,314,850,000.00 ililipwa kwenye akaunti nane za wateja tofauti na siyo kubebwa kwenye viroba au magunia.
Na zile zilizotoka toka benki ya Stanbic zilizotajwa hapo juu zilitumwa kwa njia ya TISS na siyo kubeba kwenye magunia au viroba.
4.4 Malipo kwa mfanyakazi wa benki ya Mkombozi
Gazeti la Mawio la tarehe 20-26, Novemba, 2014 tolea namba 0122 liliandika kuwa mwanasheria wa benki ya Mkombozi ajulikanaye kwa jina la Rweyengeza Alfred alipokea malipo toka akaunti ya VIP ya shilingi milioni 40.2.
Benki inatoa tamko kuwa haina mfanyakazi anayetambuliwa kwa jina hilo na wala hakuna mfanyakazi yeyote wa benki aliyelipwa fedha toka kwenye akaunti ya VIP.
Wito kwa umma
Benki ya Mkombozi inachukua fursa hii kuwatarifu wateja wake na umma kutopotoshwa na taarifa au tuhumma zilizofafanuliwa hapo juu na kuwataka wateja wake wote kutokuwa na hofu yeyote kwani benki ipo imara na inafanya kazi kwa kufuata misingi ya sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa na Benki Kuu ya Tanzania. Benki inawataarifu wateja wake na Watanzania kwa ujumla kutoyumbishwa na tuhumma hizo ambazo hazina ukweli ndani yake na badala yake waitumie benki yao kwa shughuli za maendeleo ya nchi yetu.
Pamoja tunajenga nchi na uchumi wa nchi yetu.
Hitimisho
Benki ya biashara ya Mkombozi haijihusishi na haitajihusisha na utakasishaji wa fedha chafu.
Imetolewa na:
MKURUGENZI MTENDAJI BENKI YA BIASHARA YA MKOMBOZI
Ni vizuri kujitetea lakini ukweli na nyinyi mnahusika na uizi huo kama bank.
ReplyDeleteNi sawa kujitetea lakini ukweli unabaki pale pale na nyinyi mnahusika kwenye uizi huu kwa namna moja au nyingine.
ReplyDeleteTatizo sio benki ila hao wenye benki yao yaani maaskofu wa kikatoliki kutumbua mipesa ya waumini wao bila kujali kuwa hospitali hazina dawa,yaani sioni hata umuhimu wa dini kama wachungaji wenyewe ndio wanaotafuna malishio ya kondoo wao!
ReplyDeleteMaaskofu wa kikatoliki mnatutia aibu wakristo wenzenu!