Paul Makonda: Vurugu za Mdahalo zilizima Ndoto Zangu

 Katibu wa Hamasa wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Paul Makonda amesema alitamani kuzungumza siku ya mdahalo ulioandaliwa na Kigoda cha Mwalimu Nyerere Foundation lakini vurugu zikazima ndoto yake.

Makonda ambaye anatuhumiwa kuwa ndiye aliyepanga vurugu hizo zilizosababisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba kushambuliwa, alikana na kudai kuwa hata yeye alitamani kukisikia kile kilichopangwa kuzungumzwa na wasemaji wakuu wa mdahalo huo ili ajibu hoja zao katika mkutano huo.

Akizungumza jana katika ofisi za gazeti hili, Makonda alisema aliingia ukumbini akiwa na nakala ya Katiba Inayopendekezwa kwa madai kuwa ingeweza kumsaidia kuainisha yale ambayo yangejadiliwa na ikibidi achangie hoja kwa kutetea au kutoa ufafanuzi wa kile kilichoandikwa ndani ya Katiba hiyo.

“Nasikitika kwa sababu malengo yangu hayakutimia kutokana na vurugu zile. Lengo langu lilikuwa; nipate nafasi ya kuzungumza ili nitoe hoja zangu na kufafanua uzuri wa Katiba Inayopendekezwa,” alisema.

Hata hivyo, alisema yaliyosemwa na Jaji Warioba kabla ya mdahalo kuvunjika, yalimpa fursa ya kujua ni vifungu vipi vina kasoro na vipi viko sahihi.

“Kwa maelezo ya Jaji Warioba, asilimia 90 ya maoni yaliyokuwamo katika Rasimu waliyoipendekeza ndiyo yaliyomo katika Katiba hii Inayopendekezwa,” alisema Makonda.

Tuhuma zinazomwandama

Kada huyo wa CCM, akizungumzia tuhuma kuwa alishiriki kumpiga Jaji Warioba, alisema kamwe hawezi kufanya kitu kama hicho na hakuna mtu yeyote anayeweza kuthubutu kumpiga mzee huyo.

Alisema tuhuma zinazozidi kumwandama sasa ni mwendelezo wa zile zilizokuwa zikiwatuhumu awali, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.

“Mimi ni kama napokea kijiti kutoka kwa hawa watangulizi wangu, walishatuhumiwa sana kuwa walikuwa wakitumwa kuanzisha vurugu na mambo mengine mengi, lakini hakuna hata mtu mmoja aliyethibitisha hili, binafsi naona huu ni mchezo tu wa kisiasa wa watu kutaka kutafuta huruma kutoka kwa watu wengine,” alisema Makonda.

Alisema hata malumbano yanayoendelea hivi sasa kuhusiana na Katiba hiyo mpya, hayaihusu Tume ya Warioba bali ni baina ya vyama vya siasa vinavyotaka kujitafutia umaarufu kila kimoja kwa mtindo wake.

Alipoulizwa ni kwa nini UVCCM iliamua kutoa tamko linaloashiria kuanza kwa mapambano ya kuhakikisha Katiba hiyo inapita kwa kupigiwa kura ya ndiyo na Watanzania wote, Makonda alisema: “Mimi kama msemaji wa UVCCM, hatukuwahi kutoa tamko kama hilo, hii ni propaganda tu ya wapinzani wetu.” Makonda alisema daima huwa anaamini katika ukweli na siku zote hupenda kusimamia kile anachokiona kina masilahi kwa umma wa Watanzania.

Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. sasa wewe kaka hata ungepata fursa ya kuzungumza, ungezungumza nini wakati nyie ndiyo mlioipitisha hiyo katiba yenu ya ccm kinyemela pale dodoma, usitudanganye watanzania aiseeee!!!

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad