Pinda - Mjadala Escrow Umeongezwa Chumvi, Watanzania Msiamini Mambo ya Uzushi

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema taarifa nyingi za mjadala wa akaunti ya Escrow iliyofunguliwa kutokana na mgogoro wa malipo ya gharama za umeme kati ya kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) ambao unaendelea bungeni, umeongezwa chumvi na wakati ukifika Watanzania watatolewa taarifa kamili.

Kauli hiyo ya Pinda aliitoa kanisa kuu la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika wakati wa kumsimika Dk Jackson Chilongani kuwa Askofu wa Sita wa dayosisi hiyo.

Awali, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Jacob Chimeledya aliitaka Serikali kutoa taarifa juu ya akaunti ya Escrow ili wananchi wajue kilichotokea ili ijulikane ukweli upi na uvumi upi kwani iko hatari ya kutengeneza taifa lenye kuamini uvumi.

Dk Chimeledya alisema Watanzania sasa wanaishi kwenye hali ya sintofahamu kwani hawajui yupi anasema ukweli na yupi ni `mzushi’. Alisema ni lazima Serikali itoe maelezo kwa wananchi juu ya kashfa hiyo ili wajue kilichotokea kwani ipo hatari ya kutengeneza taifa linaloishi kwa kuamini uvumi.

“Hatutakiwi kuishi kwenye taifa linaloamini uvumi… taifa halitapiga hatua kwa taarifa za kusikia tu bila kujua ukweli uko wapi, nini kimetokea na hatua gani imechukuliwa,” alisema
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad