Ni kwa takribani miezi 5 sasa imepita tangu kuibuliwa kwa sakata la ufisadi wa mabilioni ya ESCROW account,kashfa iliyoibuliwa na mbunge wa Kigoma Kusini Davidi Kafulila,kashfa iliyoibua mzozomkubwa bungeni kiasi cha mwanasheria mkuu jaji Fredrick Werema kudaiwa kutoa kauli za kumtishia maisha mh Kafulila ikiwa ni pamoja na kumwita Tumbili,huku akikanusha kwa nguvu zote kwamba fedha hizo za ESCROW zilizotokana na mzozo wa kibiashara kati ya IPTL na TANESCO si za umma bali ni za IPTL na wadau wenzake wa kibiashara.
Sasa kashfa hiyo imeibuka upya na kwa nguvu zote,hasa ikichagizwa na mbinyo wa kibajeti,ambapo nchi wahisani wamegoma kuchangia bajeti yetu ya maendeleo mpaka pale ripoti hiyo itakapowekwa wazi,kinachochangia skendo hiyo kusambaa nchi nzima kama moto wa petrol ni ripoti za mkaguzi na mzibiti mkuu wa serikali na ile ya PCCB ambazo zimekwenda mbali zaidi kwa kutaja kiwango kilichochotwa kwamba ni zaidi y ash Bilioni 320,huku Bohari kuu ya madawa ikiwa haina dawa wala uwezo wa kununua dawa kutokanana kudaiwa zaidi ya bilioni 102
Nikiendelea kukumbuka mwanzoni mwa sakata la EPA, Namkumbuka aliekuwa gavana wa benki kuu Ballali akiumwa gafla na kusafirishwa gafla kwenda nchini Marekani kutibiwa, ambapo hakikupita kipindi kirefu tukatangaziwa kwamba amefariki dunia, ikumbukwe kwamba Ballali ndo aliyekuwa anajua ni nani na nani walichota mabilioni ya EPA; kwa idhini ya nani na kwa matumizi yapi,lakini ndivyo hivyo alikufa na majibu yote hayo ingawa kifo chake kilizua utata mwingi na sintofahamu, huku wakiwepo watu ambao kamwe usingewaambia Ballali amekufa wakakusikia na kukuamini.
Ni mwaka huu mwandishi wa gazeti la mwananchi Meena ndie alietutegulia kitendawili cha wapi alipozikiwa Ballali,pale alipoibuka na story hiyo ya Ballali kwa kututajia mahala alipozikwa ,akituambia kwamba mtanzania mwenzetu huyo Ballali alizikwa nchini Marekani katika eneo maarufu la makaburi nchini humo linaofahamika kama “Gate of Heaven”mwandishi huyo ama kwa kutumwa ama kujituma alienda mbali zaidi kwa kutuonesha mpaka picha za kaburi la Ballali na makaburi mengine,japo alichofeli ni kushindwa kutuwekea walau picha moja ya mwili wa Ballali ukiwa kwenye jeneza.
Kutoka EPA sasa tuna TEGETA ESCROW, yaani msitu mpya, lakini nyani wakiwa walewale,nikiwa kama mtanzania ninaeguswa na kuumizwa na athari za ufisadi na rushwa za aina yeyote kama wizi wa Richmond, EPA, ESCROW, RADA. Ninaliona zengwe lilioko mbele yetu kama taifa, hapa tutarajie kudanganywa sana, tutarajie kuhamishiwa ajenda na mwisho tutarajie propaganda nyingi kutoka serikalini kuliko ukweli. Lakini naomba nimalizie kwa kuwauliza wahusika wakuu na wahusika wadogo wa sakata la wizi wa fedha za umma kwenye account ya ESCROW na serikali kwa ujumla. Kwamba safari hii je, wezi wa pesa zetu watapelekwa mahakamani? Ama wataumwa gafla na kukimbilia kutibiwa ughaibuni kama alivyofanya Balali? Je, watuhumiwa wakijifisha ama kufishwa watazikwa safari hii nyumbani Tanzania ili nami nipande treni kutoka kwetu Kigoma walau niwahi matanga? Ama ni kama kawaida watazikiwa ughaibuni (Marekani)mnijibu kiungwana tafadhari, watazikwa Bongo ama kwenye makaburi ya Gate of Heaven kama Ballali?