MBUNGE wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM), amesema licha ya kulishwa sumu na watu asiowajua hatohama Tanzania kama anavyoshauriwa.
Mkono, pia amegoma kuzungumzia sakata la IPTL na akaunti ya Escrow hadi apate kibali cha Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema.
Kauli hiyo aliitoa jijini Dar es Salaam jana, alipozungumza na waandishi wa habari juu ya tukio la kulishwa sumu na kulazwa hospitalini nchini Uingereza.
Mkono, alisema Novemba 11 mwaka huu akiwa na wabunge wenzake wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, walikwenda nchini Uingereza kwa ziara ya kikazi, ambako alipofika huko aliugua ghafla na kukimbizwa hospitali.
Alisema akiwa hospitali, wabunge wenzake wakiongozwa na Mwenyekiti William Ngeleja, waliwasiliana na ndugu zake juu ya tukio hilo na waliwapa maelekezo ya kuwasiliana na daktari wake (Mkono), Dk. Kapteni
Mkono, alisema Dk. Kapteni anayefanya kazi hospitali ya TMJ, aliwaelekeza wenzake dawa za kumpa kwa kuwa alihisi amelishwa sumu.
“Ukweli nimelishwa sumu, madaktari wameshathibitisha jambo hilo…sijui kina nani walionifanyia hivi, uchunguzi wa aina ya sumu na mtu aliyenipa bado vinaendelea…, waliotenda hivi wanajidanganya,” alisema.
Mkono, alisema akiwa jijini Dar es Salaam alitumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms), ikimtahadharisha juu ya safari yake na madhara atakayoyapata.
Alisema baada ya kutumiwa ujumbe huo, aliwaonyesha wenzake ambao walimtia moyo na kumtaka awe muangalifu na nyendo zake.
Mkono, alisema ujumbe huo utakuwa ni sehemu ya uchunguzi wa tukio lake aliloliita ni la kihuni, lilifanywa na wahuni wasiomtisha.
“Nimeshauriwa nihame Tanzania kwa kuwa tumefikia hatua mbaya, lakini mimi nimesema sihami kwa sababu ya wahuni wachache,” alisema.
Alibainisha kulishwa sumu kwa wabunge si jambo geni hapa nchini, kwa kuwa hata Waziri wa Uchukuzi Dk. Harisson Mwakyembe, alifanyiwa hivyo na kukimbizwa nje ya nchi kwa matibabu.
Kuhusu IPTL
Hata hivyo, Mkono hakuwa tayari kuzungumzia tukio la kulishwa sumu na sakata la IPTL linaloendelea bungeni, ingawa alisema kuna watu anawahisi kuhusika.
Alisema kuwa, alianza kushiriki kesi za IPTL mwaka 1997 akiliwakilisha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), na kila kitu kilifanyika kwa uwazi na kipo kwenye mitandao.
Mkono, alisema hawezi kuzungumzia masuala ya IPTL bila kibali cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kwa sababu kazi aliyoifanya alipewa na serikali.
Alisema kwa mujibu wa maadili ya uwakili, hapaswi kutoa siri au jambo lolote la mteja wake bila kibali kutoka kwa mhusika.
Polisi wagoma
Jana, Tanzania Daima lilipata habari kwamba polisi walimuhoji Mkono juu ya madai ya kulishwa sumu.
Gazeti hili liliwasiliana na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mrakibu Mwandamizi (SSP), Advera Senso, ili kufahamu kuhusu mahojiano hayo, ambako hakuwa tayari kuweka wazi na aliomba kupewa taarifa zaidi askari waliomuhoji Mkono walitokea wapi.
“Ni vyema ukajiridhisha kwanza kama hao askari wanatokea hapa kwetu au wanatoka kanda maalum …maana inaweza kuwa askari hao wanatimiza wajibu wao wa kawaida wa majukumu ya kazi hivyo jiridhishe halafu unipigie tena,” alisema.
Tanzania Daima halikuishia hapo, liliwasiliana na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna (CP), Suleiman Kova, ambaye alitaka kujua eneo alilopewa sumu hiyo.
“Naomba unieleze mahali au eneo alilonyweshwa sumu ili nijaribu kufuatilia au ameiripoti wapi hiyo taarifa maana sasa sina taarifa,” alisema.
Tanzania Daima