Wapinzani Wamsulubu Mwakyembe Bungeni

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, jana ilimsulubu Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ikieleza kuwa wizara yake iliingia mkataba wa mradi wa treni za kisasa kutoka Stesheni ya Dar es Salaam hadi Pugu kupitia Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) bila kufuata taratibu.

Kambi hiyo ililieleza Bunge kuwa mkataba huo ulisainiwa baina ya mmiliki wa Kampuni ya M/s Shumoja, Robert Shumake na Shirika la Reli Tanzania huku Waziri Mwakyembe akishuhudia.

Msemaji Mkuu wa kambi hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu,  Uwekezaji na Uwezeshaji, Pauline Gekul alitoa madai hayo wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu muswada wa marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP).

Gekul alisema taratibu hazikufuatwa kwa kuwa haieleweki ni lini Serikali, wakala au Wizara ya Uchukuzi ilitangaza zabuni ya mradi wa treni kutoka Stesheni hadi Pugu kupitia JNIA.

“Pia haijulikani ni lini Serikali ilifanya upembuzi yakinifu kuhusu mradi huo wa reli kwa kufuata taratibu kama zinavyoainishwa na Sheria ya PPP ya mwaka 2010 ambayo inafanyiwa marekebisho hivi sasa,” alisema Gekul na kuongeza: “Haijulikani ni kampuni ngapi ambazo ziliomba tenda ya ukandarasi wa treni na kwamba M/s Shumoja ilishinda tenda hiyo kwa vigezo gani.”

Alisema kwa kifupi ni wazi kuwa Dk Mwakyembe na wizara yake walikiuka vifungu vya Sheria ya PPP. Alivitaja vifungu hivyo kuwa ni 4(1) na (2) vinavyomtaka waziri kutangaza katika Gazeti la Serikali miradi mbalimbali inayotegemewa kufanywa na sekta ya umma kwa ubia na sekta binafsi.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad