TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu waandishi wa habari, Tumewaomba kukutana nanyi hapa leo baada ya kupata fununu kuwa Rais Jakaya Kikwete anataka kutumia hotuba yake ya kesho na wanaoitwa, “Wazee wa Dar es Salaam” kutetea wizi mkubwa wa fedha za umma uliofanyika ndani ya Benki Kuu (BoT), kupitia Akaunti ya Tegeta Escrow.
Tunazo taarifa kuwa Rais Kikwete amejipanga kuuhadaa umma kwa kisingizio cha uchunguzi wa Ikulu, ili kuwalinda watuhumiwa ambao wanapaswa kuwajibishwa kwa kuwafuta kazi, kushitakiwa na kufilisiwa. Habari tulizozipata kutoka ndani ya Ikulu kwenyewe, zinasema Rais Kikwete amejiandaa kumlinda Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi.
Tunapenda kumtahadharisha Rais Kikwete kuachana mara moja na mpango wowote wa kumlinda Profesa Muhongo na Maswi, ambao hadi muda huu walipaswa siyo kuwa nje ya ofisi, bali walitakiwa kuwako gerezani.
Ndugu waandishi wa habari; Umma unafahamu kwamba anayejiita mmiliki wa Kampuni ya PAP, alikabidhiwa fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Escrow, kabla ya kuwa mmiliki halali wa kampuni hiyo.
Ushahidi wa hili, unapatikana katika kesi iliyofunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania na James Rugemalira, dhidi ya Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof. Benno Ndulu, Kampuni ya PAP na Benki ya Stanbic, tawi la Tanzania. Rugemalira alifungua shauri hili baada ya kukuta fedha zilizokuwapo kwenye akaunti ya Escrow zimeshachukuliwa, wakati yeye akiwa bado hajamaliziwa kiasi chake cha fedha alichokuwa anadai baada ya kuuza asilimia 30 ya hisa zake katika IPTL.
Katika shauri hilo lililomalizika kwa njia ya usuluhishi wa mahakama, Mahakama Kuu ya Tanzania, pamoja na mengine, ilisema yafuatayo:
·Kwamba baada ya kampuni ya VIP kulipwa fedha zake zilizotajwa katika mkataba, itailipa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) kodi yote ya mapato inayotokana na mkataba inayofikia Sh. 38, 186,584,322/- (bilioni thelathini na nane milioni mia moja na themani na sita laki tano na elfu themanini na nne na mia tatu ishirini na mbili) kama zilivyokadiriwa na TRA kupitia Kadirio la Kodi Na. 427038820 la tarehe 15 Januari 2014.
Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani tarehe 8 Januari 2014 na VIP ENGINEERING AND MARKETING LIMITED (VIP) kama mdai na iliunganisha kesi za madai Na. 49/ 2002 na kesi ndogo Na. 254 YA 2003.
· Kwamba baada ya VIP kulipa kodi hiyo kwa TRA, fedha zake zilizobaki hazitalipwa kwake mpaka pale itakapowasilisha Cheti cha Kulipa Kodi na hati za kuhamisha asilimia 30 ya hisa zake katika IPTL kwa mwanasheria wa PAP, na wasilisho hilo lilitakiwa kufanyika kabla ya saa 10 jioni ya tarehe 27 Januari 2014.
·Aidha, baada ya kulipwa kiwango chote cha mkataba kilichotajwa hapo juu, VIP itathibitisha uridhiaji na ukubali wake wa kuhamishwa asilimia 70 ya hisa za MECHMAR CORPORATION (MALAYSIA) BERHAD katika IPTL, na uridhiaji na ukubali huo unarudishwa nyuma kuanzia tarehe ya mauzo na uhamishaji wa hisa hizo kwa PAP.
Ndugu waandishi wa habari; Hii maana yake nini? Jibu ni kwamba, wakati PAP analipwa kiasi cha Sh. 321 bilioni kutoka BoT, haikuwa mmiliki halali wa IPTL. Hakuwahi kusajili hisa zake BRELA wala hakuwa amenunua asimia 30 ya hisa za VIP.
Huu ni wizi ambao hauwezi kuvumiliwa na umma na chama chetu, ambacho ni tegemeo la Watanzania katika kulinda rasimaliza za taifa, ikiwamo fedha na kutetea haki za wanyonge na kusimamia misingi ya uwajibikaji, hakiwezi kunyamaza na kumuacha Rais Kikwete akitekeleza mradi wake wa kulinda wezi.
Hakiwezi! Kwa msingi huo, tunamtaka Rais Kikwete katika hotuba yake ya kesho, kuwajibisha wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine, katika kutekeleza wizi huo. Miongoni mwao, ni Prof. Muhongo, Maswi, Gavana wa BoT, Prof. Ndulu, Katibu Mkuu wizara ya Fedha, Silviacius Likwelile, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredric Werema na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felicesmi Mramba.
Ndugu waandishi wa habari, Watanzania bado wanakumbuka kauli iliyotolewa bungeni wakati wa mkutano uliopita kuwa familia ya Rais Kikwete nayo iko nyuma ya sakata hili ikiwa mnufaikaji mkubwa kupitia kwa mtu aitwaye Albert Marwa ambaye ana uhusiano na familia hiyo.
Kitendo cha Rais Kikwete kushindwa kuchukua hatua madhubuti katika jambo hili, utakuwa ni ushahidi wa wazi kuwa kigugumizi ambacho kimekuwa kikiikabili serikali yake katika jambo hili kinasukumwa na jambo kubwa nyuma yake, ikiwamo kujilinda binafsi na kulinda familia yake.
Ndugu waandishi wa habari, Suala la miamala iliyofanyika kupitia Benki ya Stanbic katika sehemu ya kashfa hiyo ya Akaunti ya Escrow, si suala la kufanyia mzaha au kupuuzwa hata kidogo katika ufisadi huu.
Ni kupitia benki hiyo ndiko kiwango kikubwa cha fedha zaidi ya Sh. 160 bilioni, zilibebwa kwa magunia, malumbesa na sandarusi ndani ya siku moja mchana kweupe, tena tunaambiwa wengine walikwenda kwa magari yenye nambari za serikali na fedha hizo zilipelekwa Ikulu ambako Rais Kikwete anafanyia kazi na kuishi.
Ni ukweli ulio wazi kuwa hakuna benki ndani ya nchi yetu inayoweza kufanya miamala ya mabilioni ya fedha kwa kiwango hicho, bila BoT kuidhinisha. Kwa mantiki hiyo hiyo, Gavana Prof. Ndulu hawezi kukwepa uwajibikaji kwenye jambo hili zito kwa kuwa alilifahamu na kulilidhia.
Tunatarajia Rais Kikwete ataueleza umma wa Watanzania hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi hawa wa umma na siyo kuja na visingizio vya miamala iliyochukuliwa katika Benki ya Mkombozi pekee. Watanzania wanasubiri kusikia Rais Kikwete anachukua hatua dhidi ya Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum ambaye wakati fedha zinaztolewa katika Akaunti ya Escrow kati ya Septemba na Desemba mwaka jana, alikuwa ndiye Kaimu Waziri wa Fedha.
Wakati huo, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa alikuwa Afrika Kusini kwenye matibabu ya ugonjwa uliopelekea kifo chake ambacho hadi leo kimeendelea kudaiwa kuwa na utata.
Ndugu waandishi wa habari; Aidha, katika kuwatafuta watu waliochukua fedha za Akaunti ya Escrow kwa magunia na malumbesa, Rais Kikwete aweke wazi kile kinachoonekana ushirika wa ufisadi kati ya serikali, Benki ya Stanbic na chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana.
Tunazo taarifa za uhakika kwamba Kinana alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo na Mjumbe wa Bodi ya Stanbic, na ambaye amekuwa kiunganishi kikubwa kati ya serikali, CCM na benki hiyo katika kufanya miamala ya aina hiyo ya kifisadi.
Umma wa Watanzania unamtarajia Rais Kikwete amwagize Kinana, kwa ushawishi wake alionao ndani ya Stanbic, awataje watu waliokwenda kuchukua mabilioni ya fedha kwa malumbesa, magunia na sandarusi, vinginevyo atakuwa anahalalisha madai haya kuwa ushirikiano huu una kitu nyuma na kwamba, fedha kutoka Akaunti ya Escrow ya Tegeta, kupitishiwa benki hiyo halikuwa jambo la bahati mbaya.
………………………
Arcado Ntagazwa
MWENYEKITI WA BODI YA WADHAMINI CHADEMA