Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mwanamume mmoja amewafyatulia risasi watu wawili na kusababisha kifo cha mmoja kwa kile kinachodaiwa kumletea usumbufu wakati wa mkesha wa harusi.
Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Ilala, David Mnyambuga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ingawa hakuwa tayari kulizungumzia kwa madai kuwa siyo msemaji na anayetakiwa kufanya hivyo ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala ambaye hakupatikana kulizungumzia hilo.
Majeruhi wa tukio hilo, Goodluck Madaraka aliyejeruhiwa na risasi zilipokuwa zinapigwa hewani, alisema saa tano na nusu usiku walipokuwa wanacheza muziki kwenye mkesha wa harusi, ghafla jirani yao aliyefahamika kwa jina la Lucas Muhabe alikuja na panga na kuwafukuza kwa madai kuwa wanampigia kelele.
Alisema Muhabe aliondoka na baada ya muda alirudi na bastola na kupiga risasi ovyo na kwa bahati mbaya ikampata begani Mahamudu Muhasi aliyekuwa anapita njia na kumpiga nyingine ya kichwa na kumuua papo hapo.
“Muhasi alikuwa anapita njia hivyo hata vijana walivyokimbia yeye hakukimbia na alipopigwa risasi ya bega la kushoto alilalama kumwambia huyo baba kuwa anamwonea kwani hafahamu kitu chochote, cha kushangaza baada ya kuambiwa hivyo aligeuka na kumpiga nyingine ya kichwa na kufariki dunia papo hapo,” alisema Madaraka.
Madaraka alisema kuwa kwenye heka heka za kupigwa risasi hizo moja ilimpitia kwenye shavu na kumpasua na alikwenda Hospitali ya Amana na kushonwa nyuzi tatu.
Kaka wa marehemu, Salim Ally alisema kuwa Muhasi alikuwa anashinda kwake na kulala kwa mjomba wake mbali kidogo kutoka kwake, siku ya tukio baada ya kula chakula cha usiku na kuzungumza hadi saa tano usiku, alimsindikiza.
Alisema alipohakikisha wamepita kwenye maeneo ambayo hakuamini kama ni salama, alimwacha aende mwenyewe, njia kuu ikiwa ni hapo palipokuwa na mkesha wa harusi na alipata taarifa ndugu yake ameuawa kwa kupigwa risasi.
Kelele za Harusi Zaua Mpita Njia Kwa Risasi D’Salaam
0
December 27, 2014
Tags