Kikwete ana wakati mgumu akijaribu kupuuza maazimio ya Bunge

Maazimio ya Bunge yalimtaka Rais kuwawajibisha wote waliotajwa kuhusika na kashfa ya escrow, uamuzi ambao upo mikononi mwa Rais Kikwete

Hatimaye Novemba 29, 2014 Bunge letu lilimaliza kikao muhimu sana pengine kuliko vikao vyote tangu lianze mwaka 2010.

Katika makala haya, ninafanya tathimini ya yale yaliyojiri katika vikao vya 16 na 17 vya Bunge letu kwa kuzingatia mafunzo yaliyojitokeza katika Bunge hili katika maeneo matatu, ambayo ni mamlaka ya Bunge, kukua kwa demokrasia na nafasi ya kizazi kipya cha wanasiasa.

Mamlaka ya Bunge.

Baada ya wabunge kutoa maoni yao katika Taarifa iliyowasilishwa na Kamati ya Hesabu ya Serikali (PAC) na majibu ya Serikali kama yalivyowasilishwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ilikuwa ni wazi kwamba Serikali ilikuwa imelemewa na hoja za PAC.

Kulemewa kwa hoja za Serikali kulikuja kuwa wazi zaidi baada ya Kamati ya PAC kujibu kwa umakini mkubwa hoja za Serikali na wabunge waliokuwa wanaegemea upande wa Serikali.

Baada ya mjadala kuhitimishwa mambo matatu yalikuwa dhahiri kwa wabunge wengi. Mosi, sehemu ya fedha zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow ilikuwa ni ya umma.

Pili, kuna baadhi ya viongozi wa Serikali na watu wengine wenye mamlaka katika jamii walikuwa wamejipatia fedha ya Escrow katika mazingira yanayotia shaka kuhusu maadili yao kama viongozi.

Tatu, Serikali haikutekeleza wajibu wake kikamilifu katika kusimamia masilahi ya umma katika uendeshaji wa akaunti ya Tegeta Escrow na mikataba ya nishati kwa jumla.

Kutokana na makosa haya ilikuwa lazima kwa Bunge kuchukua hatua kadhaa katika kuiwajibisha Serikali na hapa ndipo hoja ya mamlaka ya Bunge inapokuja.

Kutokana na mjadala wa Bunge usiku wa Ijumaa 28 Novemba 2014 ilikuwa wazi kwamba Bunge letu limewekewa mipaka mikubwa sana kikatiba katika kuiwajibisha Serikali.

Pamoja na kwamba wabunge wengi walitamani kwa usahihi kabisa kuwajibisha mara moja waliohusika na kadhia hii, lakini walikuwa hawana uwezo wa kikatiba wa kutekeleza matamanio yao.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad