Mechi ya Mtani Jembe nchini Tanzania, inayozikutanisha timu mbili za jijini Dar es Salaam zenye ushindani wa jadi, za Simba na Yanga imegeuka uwanja wa machinjio kwa makocha wa Yanga kwa mara ya pili mfululizo.
Mechi kama hiyo ilipofanyika mwaka jana, 2013, Yanga ilifungwa magoli 3-1 na kusababisha aliyekuwa kocha wake Ernie Brandts kutimuliwa pamoja na benchi lake la ufundi. Mwaka huu ni zamu ya kocha Marcio Maximo kufungashiwa virago vyake baada ya kunyukwa mabao 2-0 katika mechi ya Mtani Jembe iliyofanyika Jumamosi iliyopita katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, na huu ukiwa ni mchezo wa nane wa ushindani baada ya michezo saba tu ya ligi kuu ya Vodacom ya nchi hiyo.
KOCHA Maximo ambaye alipokelewa kwa vifijo na nderemo na mashabiki na wanachama wa Yanga mwezi Juni mwaka huu baada ya kutangazwa kuwa kocha mpya wa timu yao, amewaaga rasmi wachezaji wa timu hiyo kwenye mazoezi uwanja wa Sekondari ya Loyola ya jijini Dar es Salaam.
Mazoezi hayo ya Jumanne asubuhi yaligeuka simanzi baada ya Maximo kuwakusanya wachezaji wake na kuwambia kuwa kuanzia hiyo jana hakuwa kocha wa timu hiyo tena na kuwatakia maisha mema ndani ya klabu hiyo ya Jangwani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wachezaji wa klabu hiyo walielezea kutoridhishwa na uamuzi wa uongozi wa klabu hiyo kumuacha kocha wao na mshambuliaji Hamis Kiiza kutoka Uganda.
Mmoja wa wachezaji hao alisema "Ni kweli kocha ametuaga asubuhi daa! ndio hivyo tumesikitika lakini hatuna jinsi."
Naye mchezaji mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema "Inaumiza sana jana (juzi) tumefanya nae mazoezi vizuri kabisa tena amechangamka kama kawaida kumbe nyuma kuna mambo yanaendelea, leo asubuhi tumeenda mazoezi kama kawaida tukijua tunafanya mazoezi matokeo yake anasema acheni kila kitu kaeni hapo nataka kuzungumza na nyinyi".
Mchezaji mwingine wa timu hiyo alisema "Hakuna mchezaji kwa kweli aliyependezwa na kitendo cha uongozi, yaani kwenye mazoezi asubuhi ilikuwa kama msiba, 'mood' ya kufanya mazoezi iilisha kabisa, yaani hakuna aliyekuwa na hamu ya kuendelea na mazoezi.
"Tumefanya kidogo mazoezi tukaondoka, ukiangalia ni sawa tumefungwa cha muhimu ilikuwa ni kukaa chini na kuzungumza na kuangalia cha kufanya, kama kuna mapungufu basi yafanyiwe kazi, mimi sijaona haja ya kumfukuza kocha hasa kipindi kama hichi."
Meneja wa timu hiyo Hafidhi Saleh alikiri Maximo kuwaaga wachezaji kabla ya mazoezi ya timu hiyo kwanza akiwapa moyo wajitume kwa kuwa ni wachezaji wazuri na timu ni nzuri na kuwataka kuongeza bidii ili wafike mbali.
"Kwa kweli inasikitisha hakuna mchezaji wala mtu aliyefurahia, kama yupo labda kimoyomoyo ila dah imetuumiza, ni mazoea cha muhimu tugange yajayo hayo mengine tuwaachie viongozi."alisema Saleh
Mchezo wa Mtani Jembe ambao ni wa kujifurahisha na kuongeza utani kati ya timu hizo, umegeuka kuwa kipimo cha ubora wa kocha hata kama kocha huyo anafanya vizuri katika michezo ya ligi kuu. Hadi wakati anafukuzwa, kocha wa Yanga Mbrazil Marcio Maximo, timu yake inashika nafasi ya pili baada ya Mtibwa inayoongoza katika msimamo wa ligi hiyo kutokana na michezo saba tu iliyochezwa.
Baadhi ya mashabiki wameunga mkono uamuzi wa kumtimua Maximo wakisema timu haikuwa na uwezo wa kupambana na timu pinzani, huku wengine wakipinga uamuzi huo kuwa haukustahili kuhukumu uwezo wa kocha huyo katika mchezo mmoja wa kirafiki na kusahau nafasi inayoshikiliwa na timu katika msimamo wa ligi kuu.
Bora alivyoondolewa, kocha bomu kabisa!
ReplyDelete